POLISI SIHA WAOMBA USHIRIKIANO WA MADIWANI KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.

Geofrey Stephen
3 Min Read

Siha, Kilimanjaro

Jeshi la Polisi Wilaya ya Siha limewaomba madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kushirikiana kikamilifu na jamii katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyowalenga wanawake na watoto.

Habari Picha 6593

Wito huo umetolewa na Daniel Nyolobi kutoka Jeshi la Polisi Sanya Juu kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Siha, Zakia Shuma, wakati akiwasilisha tathmini ya hali ya uhalifu katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Siha kilichofanyika katika ukumbi wa halm.ashauri hiyo

Habari Picha 6594

Akizungumza Januari 30, 2026, Nyolobi amesema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado vipo kwenye jamii, na juhudi za pamoja zinahitajika ili kuvikomesha. Ameeleza kuwa makosa hayo ni pamoja na ubakaji, ulawiti na vitendo vingine vinavyokiuka maadili ya binadamu.
“Matukio haya yapo kwenye jamii zetu. Ili kuwanusuru watoto na wanawake, ni lazima tushirikiane kwa umoja kupiga vita ukatili huu na kuwajengea watoto uwezo wa kujilinda dhidi ya watu wenye nia ovu,” amesema Nyolobi.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii, kuanzia ngazi ya familia hadi viongozi wa serikali za mitaa na madiwani, kuhakikisha wanatoa taarifa za matukio ya ukatili mara yanapotokea ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa haraka.

Nyolobi ameongeza kuwa mara nyingi wahusika wa matukio hayo huwa ni ndugu au watu wa karibu, jambo linalosababisha baadhi ya matukio kufichwa.

“Tukiendelea kuwaficha wahusika kwa sababu tunawafahamu, vitendo hivi haviwezi kuisha. Ni lazima tuwe wazi na tushirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine,” amesisitiza.

Habari Picha 6553

Aidha, ameeleza kuwa pamoja na makosa ya ukatili wa kijinsia, wilaya hiyo pia inakabiliwa na makosa mengine kama uhalifu wa kifedha, migogoro ya mali, na makosa yanayohusiana na maadili ya jamii.
Takwimu za Matukio

Kwa mujibu wa taarifa hiyo:
Matukio ya ubakaji
2024: Matukio 40
2025: Matukio 19
Matukio ya ulawiti
2024: Matukio 11
2025: Matukio 5

Takwimu hizo zinaonesha kupungua kwa matukio hayo, lakini Jeshi la Polisi linasisitiza kuwa bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuyatokomeza kabisa.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Dancani Urasa, amesema baraza limezipokea taarifa hizo na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na jamii kwa ujumla.
Amesema lengo ni kuhakikisha jamii inakuwa salama na kulinda wanawake na watoto dhidi ya watu wenye nia ovu.

 

Mwishoo……

Share This Article
Leave a Comment