ZARA TOURS YANG’ARA TENA SERENGETI, YAUTHIBITISHA UBORA WAKE KWA KUTWAA NA KUENDELEZA HESHIMA KATIKA TUZO ZA KIMATAIFA

Geofrey Stephen
4 Min Read

Geofrey Stephen . Arusha

Kampuni ya utalii ya Zara Tours yenye makao yake makuu mjini Moshi imeendelea kudhihirisha ubora wake katika sekta ya utalii baada ya kunyakua tuzo nyingine muhimu katika hafla ya kifahari ya Serengeti Awards.

Ushindi huo ni muendelezo wa mfululizo wa tuzo ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizipata karibu kila mwaka, ishara ya uthabiti wake katika kutoa huduma za viwango vya kimataifa.

Tuzo hiyo ilikuwa miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa katika hafla kubwa iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha.

Habari Picha 6588

Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wakuu wa utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiweka jukwaa la kutambua mchango wa sekta hiyo katika uchumi na maendeleo ya taifa.

Serikali Yapongeza Sekta ya Utalii.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye aliipongeza sekta ya utalii kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira, pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kama kivutio bora cha utalii.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau binafsi umeendelea kuleta matokeo chanya, hasa katika kuboresha miundombinu na huduma zinazowawezesha watalii kupata uzoefu bora wanapotembelea vivutio vya nchi.
Zara Tours:

Mafanikio Yanayotokana na Ushirikiano.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Zara Tours, Bi. Zainabu Ansell, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa ya timu, mshikamano wa ndani ya kampuni na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wadau wa sekta ya utalii.

Habari Picha 6589

Alieleza kuwa maboresho yanayoonekana katika Mlima Kilimanjaro ni ushahidi wa wazi wa jitihada za pamoja za kulinda na kuendeleza rasilimali za taifa.

“Mazingira ya mlima yameimarika, huduma zimeboreshwa na hali ya usalama imeongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo linalowapa watalii uzoefu wa kipekee,” alisema Bi. Zainabu.

Kilimanjaro Yazidi Kuitangaza Tanzania Duniani.

Kwa mujibu wa Bi. Zainabu, Mlima Kilimanjaro umeendelea kuwa alama muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa, na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa vinara wa utalii wa mlima barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Alibainisha kuwa ongezeko la watalii wanaopanda mlima huo limechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii na kuongeza mapato ya taifa. Kampuni kama Zara Tours zimekuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha wageni wanapata huduma salama, zenye ubora wa hali ya juu na zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Habari Picha 6590

“Ninajivunia sana mafanikio haya. Leo ni siku ya kusherehekea hatua tulizofikia. Mimi pamoja na timu yangu tumejipanga kikamilifu kuendelea kuboresha viwango vya kitaaluma, kuongeza ubunifu na kuhakikisha wageni wengi zaidi wanavutiwa kuja kuupanda Mlima Kilimanjaro,” alisisitiza.

Ahadi ya Utalii Endelevu.

Bi. Zainabu aliahidi kuwa Zara Tours itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kukuza utalii endelevu, kulinda mazingira na kulitangaza taifa la Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Hafla ya Serengeti Awards imelenga kutambua na kuthamini mchango wa taasisi, makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini  na ushindi wa Zara Tours ni kielelezo cha ubora unaoendelea kuijenga taswira ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment