MADIWANI WAPYA SIHA WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA UKUSANYAJI WA MAPATO.

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Bahati Siha .

Madiwani wapya wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendeleza juhudi za ukusanyaji wa mapato na kuibua vyanzo vipya, ili kudumisha na kuongeza kasi ya maendeleo wilayani humo.

Wito huo umetolewa na Poncean Kilumbi, mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakati wa Baraza la Kawaida la Madiwani wa Halmashauri ya Siha lililofanyika Januari 30, 2026.

Habari Picha 6552

Akizungumza baada ya kupata fursa katika baraza hilo, Kilumbi aliwakumbusha madiwani hao kuwa Siha ni miongoni mwa halmashauri zinazofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato mkoani humo, hivyo ni muhimu kuendeleza mafanikio hayo.

“Ni kweli, sasa muendelee pale ambapo waliopita waliacha. Walikuwa wanafanya vizuri katika maeneo mengi, hasa katika suala la ukusanyaji mapato na kuibua vyanzo vipya. Halmashauri hii ni miongoni mwa zinazofanya vizuri katika mkoa huu wa Kilimanjaro,” amesema Kilumbi.

Habari Picha 6553
Habari Picha 6554

Amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ni nguzo muhimu ya maendeleo, kwani bila mapato halmashauri haiwezi kutekeleza miradi kama ujenzi wa barabara, huduma za afya, maji na elimu.

“Suala la ukusanyaji mapato linahitaji ushirikiano mkubwa. Nimeona kwa sasa mko zaidi ya asilimia 50, jambo ambalo ni jema. Ongezeni bidii, hasa wakuu wa idara kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, ili ifikapo Juni 2026 muwe mmefikia zaidi ya asilimia 100,” ameongeza.
Kilumbi alibainisha kuwa jukumu la kukusanya mapato si la Mkurugenzi na wakuu wa idara pekee, bali pia madiwani, kwani wao wanafahamu vizuri vyanzo vya mapato katika maeneo yao.

Habari Picha 6555
Habari Picha 6556

Mikakati Yatajwa Kuvuka Lengo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha, Hellen Mwambeta, amesema halmashauri imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji mapato kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa, ikiwemo uundaji wa timu maalum.

Amesema timu hizo zinajumuisha madiwani pamoja na menejimenti, na zimekuwa zikifanya kazi kwa bidii mchana na usiku. Aidha, amepongeza mwamko wa wananchi katika kuchangia mapato, wakielewa kuwa ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Onyo kwa Wakandarasi Wanaochelewesha Miradi.

Mwambeta pia aliwataka wakandarasi wanaochelewesha miradi kukamilika kwa wakati kufuata masharti ya mikataba yao na kuzingatia sheria.

“Wakandarasi waangalie mikataba yao na watekeleze matakwa yake. Miradi ikikamilika kwa wakati, huduma zilizotarajiwa na Serikali kuwafikia wananchi zitapatikana kwa wakati,” amesema.

Usimamizi wa Miradi na Nidhamu ya Watumishi.

Awali, katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha, Dancan Urassa, amesema baraza litaendelea kusimamia kwa karibu ubora wa miradi pamoja na matumizi sahihi ya fedha za mapato ya ndani, fedha kutoka Serikali Kuu na wahisani.

Amesisitiza kuwa halmashauri haitawavumilia watumishi wazembe na itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika vituo vya huduma za jamii.

Habari Picha 6557
Habari Picha 6558

Pia amewakumbusha watumishi wa umma kutumia lugha nzuri wanapohudumia wananchi, akisema hilo ni jambo muhimu katika utoaji wa huduma bora.

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment