Na Geofrey Stephen Arusha .
Ngorongoro — moja ya maajabu ya asili ya dunia — inaelekea kuingia katika sura mpya ya uhifadhi na maendeleo ya utalii kufuatia maagizo mazito yaliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji.
Akizungumza jijini Arusha Januari 29, Dkt. Kijaji ameweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ulinzi wa Hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha mfumo wake wa ikolojia unaendelea kubaki hai, wenye mvuto wa kipekee, na salama kwa vizazi vijavyo.



Maagizo hayo yametolewa katika hafla ya kumvisha cheo Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul Razaq Badru, pamoja na uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa mamlaka hiyo.
Utalii wa Ngorongoro Kupaa Zaidi.
Mbali na uhifadhi, Serikali imeweka jicho pia katika kuboresha uzoefu wa watalii. Dkt. Kijaji amesema huduma za malazi ndani ya hifadhi zinaendelea kuimarishwa ili kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya utalii.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza idadi ya vitanda kutoka 1,555 vya sasa hadi zaidi ya 2,590, jambo litakaloongeza uwezo wa kupokea wageni wengi zaidi na kuchochea mapato ya taifa kupitia utalii.
Kila Mwaka, Kivutio Kipya!
Katika hatua ya kuifanya Ngorongoro iendelee kuwa gumzo duniani, Waziri huyo amesisitiza ubunifu katika sekta ya utalii. Amemtaka Kamishna wa Uhifadhi kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara kuhakikisha kila mwaka angalau kivutio kimoja kipya cha utalii kinaingizwa sokoni.
Hii ina maana si tu kuhifadhi kilichopo, bali pia kufikiria kesho ya utalii wa Tanzania kwa ubunifu, ubora wa huduma, na matangazo madhubuti ya vivutio vipya.
Jamii Zilizozunguka Hifadhi Zasahaulika? Hapana!
Dkt. Kijaji pia ameweka wazi kuwa mafanikio ya uhifadhi hayawezi kutenganishwa na ustawi wa wananchi wanaozunguka hifadhi. Ameagiza kuimarishwa kwa mahusiano kati ya mamlaka ya hifadhi na jamii hizo, ili nao wanufaike moja kwa moja na rasilimali za Ngorongoro kupitia ajira, fursa za kiuchumi na maendeleo ya kijamii.
Salamu Kutoka Kwa Rais.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, DC Mkude, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasilisha salamu za pongezi na heri ya Mwaka Mpya kwa viongozi na watumishi wa NCAA pamoja na wadau wa uhifadhi.
Amesema Rais ameridhishwa na ushirikiano mkubwa uliotolewa na mamlaka hiyo katika mwaka 2025, na kusisitiza kuwa mshikamano huo uendelee kwa maendeleo ya Mkoa wa Arusha na taifa kwa ujumla.



Mabeyo Amshukuru Rais, Aweka Matarajio kwa Bodi Mpya.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA, Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Venance Mabeyo,
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua tena kuongoza bodi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.
Jenerali Mabeyo pia amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kuunda bodi yenye wataalamu kutoka nyanja mbalimbali, akiwataka wakurugenzi hao wapya kufanya kazi kwa bidii na kuacha alama kama ilivyokuwa kwa bodi iliyopita.


Wakurugenzi hao wapya wamebobea katika sekta za uhifadhi, utalii, fedha na uchumi, utawala, sheria, diplomasia, utawala bora, maendeleo ya jamii, ukaguzi pamoja na teknolojia ya mifumo. Uzoefu wao katika utumishi wa umma na sekta binafsi unatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa mamlaka hiyo.
Kamishna Badru Aapishwa Rasmi.
Mapema katika hafla hiyo, Abdul-Razaq Badru alivishwa cheo na kuapishwa rasmi kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA. Ameahidi kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma kwa kiwango cha juu ili kuimarisha majukumu makuu ya Ngorongoro — uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii

DC Mkude pia amempongeza Kamishna Abdul Razaq Badru kwa kuvikwa cheo, akiahidi ushirikiano wa karibu kati ya Mkoa na NCAA, huku akihimiza kuendelea kuishi falsafa ya Rais ya 4R — Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya Taifa.
Mwisho .






