Na Geofrey Stephen.Arusha
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya, Dkt. Johannes Lukumay, ametoa wito kwa Serikali kuharakisha maboresho ya sekta ya afya nchini,
akisisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote si suala la takwimu wala sera ya kisiasa, bali ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kupata huduma bora za afya bila kujali hali yake ya kiuchumi.
Dkt. Lukumay ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa mawasiliano kati ya wananchi na Waziri wa Afya. Hafla hiyo ilifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Afya,

Mohamed Mchengerwa.
Akizungumza kwa msisitizo, Dkt. Lukumay ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unapaswa kuonekana kwa vitendo badala ya maneno. Amesema ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati, kwa ubora na bila vikwazo, hasa makundi yenye uhitaji mkubwa wakiwemo kaya maskini, watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wazee na watu wanaoishi katika mazingira magumu.
“Maana halisi ya Bima ya Afya kwa Wote ni kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali kipato chake, anapata huduma bora za afya bila kubaguliwa wala kunyanyapaliwa,” amesema Dkt. Lukumay.
Akielekeza ujumbe wake moja kwa moja kwa Waziri wa Afya, amesisitiza kuwa afya ya wananchi ndiyo msingi wa uzalishaji, ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi wa taifa. Ameonya kuwa bila wananchi wenye afya njema, malengo ya maendeleo hayawezi kufikiwa.
Dkt. Lukumay ameongeza kuwa dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuona kila Mtanzania anapata huduma bora za afya popote alipo, na kwamba Tanzania inayotakiwa ni ile ambayo wagonjwa hawateseki kwa kukosa matibabu na maskini hawabaguliwi.

Katika hotuba yake, hakusita kuibua changamoto zinazoendelea kuikabili sekta ya afya, zikiwemo upungufu wa vifaa tiba muhimu kama mashine za X-ray, ucheleweshaji wa utoaji wa fedha licha ya bajeti kupitishwa, pamoja na miradi ya afya na viwanda vya dawa kutokutumika ipasavyo.
Ametolea mfano hoja kuhusu matumizi ya bajeti ya shilingi bilioni 6.6, akitaja ucheleweshaji wa utoaji wa shilingi bilioni 1.5 kwa huduma za watoto wengi, hali inayosababisha wananchi walengwa kushindwa kupata huduma bora.
“Haina maana kununua mashine ghali halafu zinafungwa au hazifanyi kazi. Wananchi wanahitaji huduma, si majengo wala vifaa vilivyofungwa,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, uwekezaji katika sekta ya afya una faida pana zaidi ya utoaji wa tiba, kwani unachochea ajira, kuimarisha uchumi na kupunguza mateso ya wananchi.
“Maendeleo ya kweli huanza na wananchi wenye afya njema,” amesema.
Akihitimisha, amemtaka Waziri wa Afya kuhakikisha vituo vya afya vinawekewa vifaa muhimu, mashine zinafanya kazi ipasavyo na wananchi wanapata huduma.

kwa wakati bila usumbufu usio wa lazima.
Aidha, amempongeza Waziri Mchengerwa kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali wa mawasiliano kati ya wananchi na Wizara ya Afya, akisema mfumo huo utaimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika kuboresha huduma za afya.
“Tukiunganisha nguvu za serikali, chama na wananchi, tunaweza kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania,” amehitimisha Dkt. Lukumay.
Mwisho .



