Na Lucy Ngowi
NAIBU Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, amezitaka mamlaka husika ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuimarisha udhibiti wa sekta ya fedha ili kuwalinda wananchi dhidi ya mikopo kandamizi inayotolewa na taasisi zisizo rasmi, maarufu kama mikopo kausha damu.
Agizo hilo amelitoa wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea mkoani Tanga.
Amesema udhibiti madhubuti utasaidia kuzibaini taasisi na watu binafsi wanaotoa mikopo hiyo na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao, hivyo kuzuia wananchi kupoteza mali na vitu vya thamani.
Luswetula aliwaonya watoa huduma za fedha wanaokiuka sheria, ikiwemo kufanya kazi bila kusajiliwa na BoT au mamlaka nyingine husika, kuacha mara moja vitendo hivyo.
Habari Picha 10880
Aidha, amewahimiza wananchi kuhakiki uhalali wa taasisi kabla ya kukopa na kusoma kwa makini mikataba ya mikopo ili kuepuka masharti kandamizi.
Akizungumzia sekta ya fedha, amesema kumekuwepo na mafanikio baada ya maboresho yaliyofanyika, ingawa bado changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha ipo, ikiwemo matumizi ya huduma zisizo rasmi.
Amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu maadhimisho hayo katika viwanja vya Usagara, Tanga, kupata elimu ya fedha na huduma sahihi kama kuweka akiba, kukata bima na kuwekeza.
Habari Picha 10881
Pia amewataka waelimishaji wa masuala ya fedha kutoa elimu kwa lugha rahisi na kuzingatia maoni ya

wananchi ili kuboresha sera na huduma za kifedha nchini.



