Na Bahati Hai.
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Hassani Bomboko, ametoa siku tatu kwa Idara ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, kuwafuatilia watoto wadogo wanaofanya biashara ndogo ndogo ikiwemo uuzaji wa mifuko katika Soko la Sadala, na kuwasilisha taarifa kamili ofisini kwake.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 18, 2026, wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya Snow View, Bomang’ombe, kufuatia madai kwamba watoto hao wanakumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji.


Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na wananchi mbalimbali, viongozi wa Serikali akiwemo wakuu wa idara, watendaji wa kata na vijiji pamoja na viongozi wa dini, Bomboko amesisitiza vyombo husika kuchukua hatua za haraka.
“Mmesikia hapa kwamba kuna watoto wanaofanyiwa vitendo vya kinyama na vya kikatili. Ustawi wa Jamii, Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Afisa Biashara shirikianeni kwenda kulifanyia kazi jambo hili. Nawapa siku tatu nipate majibu,” amesema Bomboko.
Ameongeza kuwa ulinzi wa watoto ni msingi wa kulinda familia na jamii kwa ujumla, hivyo ni muhimu kufahamu ukweli wa taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
Mmoja wa wakazi wa Sadala, George Munisi, aliyewasilisha kero hiyo, aliomba vyombo vya usalama kufika sokoni hapo kwa kuwa watoto wadogo wanaofanya biashara ya kuuza mifuko wanadaiwa kufanyiwa vitendo viovu.
“Tunaomba sana vyombo vya usalama vifike sokoni hapa. Kuna watoto wadogo wanafanyiwa vitendo vibaya. Tukikaa kimya wataharibika,” amesema Munisi.
Mbali na kero hiyo, wananchi pia waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu katika baadhi ya shule, ubovu wa barabara, uhaba wa umeme, mrundikano wa taka, pamoja na migogoro ya ardhi. Mkuu wa Wilaya alielekeza kero hizo kushughulikiwa na idara husika.


Aidha, wakazi wa Bomang’ombe Mjini waliomba kuruhusiwa kufanya biashara kwa masaa 24, ombi ambalo Bomboko ameahidi kulifanyia kazi.
Mkazi wa Bomang’ombe, Zuli Mbaga, alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuanzisha ziara ya kutembea wilaya nzima kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
“Ni jambo jema sana kuona Serikali inawafuata wananchi walipo na kusikiliza changamoto zao. Hii inaongeza imani kwa wananchi,” amesema Mbaga.
Awali, Bomboko amesema dhamira ya ziara hiyo ni kuiondoa Serikali kwenye ofisi na kuifikisha karibu na wananchi.
“Hili ni zoezi endelevu litakaloiwezesha Serikali kufika vijijini, vitongojini na maeneo yenye mikusanyiko ya wananchi ili kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi,” amesema.
Mwisho



