Na Geofrey Stephen Arusha.
Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha umeweka msimamo mkali kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya maendeleo, ukisisitiza kuwa hakutakuwa na nyongeza ya muda kwa miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa jijini humo. Hatua hiyo inalenga kulinda thamani ya fedha za umma na kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi hiyo kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Maximilian Iranghe, amesema msimamo huo unatokana na maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, aliyefanya ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusisitiza ikamilike kwa mujibu wa ratiba bila visingizio.

Meya Iranghe amesema katika ziara hiyo ya kimkakati, Prof. Shemdoe alikagua miradi kadhaa ikiwemo Stendi ya Bondeni iliyopo Kata ya Olasiti, Uwanja wa Michezo wa Jiji la Arusha, pamoja na Soko la Kilombero, ambako alijionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa mujibu wa Meya huyo, miradi ya Stendi ya Bondeni na Soko la Kilombero imefikia takribani asilimia 40 ya utekelezaji, hatua iliyomfanya waziri kupongeza juhudi zinazofanywa huku akiwataka wasimamizi na wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa wakati. Aidha, alieleza kuwa kasi ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Jiji la Arusha imeridhisha na imepongezwa rasmi na waziri.
Iranghe amesisitiza kuwa miradi ya Stendi ya Bondeni, Soko la Kilombero, Soko la Kwa Mrombo pamoja na eneo la mapumziko imepangwa kukamilika ifikapo Mei 26, 2026, na kwamba tarehe hiyo ni ya mwisho bila uwezekano wa kuongeza muda.
“Tumepokea maelekezo ya waziri na kama Jiji tumesimama imara. Hakutakuwa na nyongeza ya muda; tutashirikiana na wakandarasi na wasimamizi kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati uliopangwa,” alisema Meya Iranghe.
Ameeleza kuwa licha ya changamoto ndogondogo zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi, hakuna sababu ya kuchelewsha kukamilika kwa miradi hiyo .
Mwisho .


