- Askofu Pallangyo: “Tumeomba Mungu Atusamehe Na Atupe Mwanzo Mpya”
- Mbunge Joshua Nasari: “Nitawatumikia Wananchi Wote—Amani Ndio Kipaumbele”
- Uongozi wa Halmashauri: “Ni Wakati wa Kazi, Sio Siasa”
- Sala za Maridhiano, Mshikamano na Baraka za Mila
- Wito kwa Taifa: “Tuzidi Kulinda Amani”
- Hitimisho: Mshikamano Chini ya Mti wa Mringaringa
Na Geofrey Stephen Meru .
Katika tukio lenye uzito wa kipekee, Askofu wa Kanisa la (AMEC) Wilaya ya Arumeru . Mkoani Arusha, akiungana na Mkuu wa Jimbo la Kati pamoja na viongozi mbalimbali wa dini, wachungaji, wazee wa mila wa jamii ya Wameru (Washili), na viongozi wa koo, wamefanya maombi maalum ya kuwaombea Watanzania waliopoteza maisha au kujeruhiwa katika vurugu za uchaguzi zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Ibada hiyo imefanyika chini ya Mti wa Mringaringa, mti wenye historia ndefu na umuhimu wa kiutamaduni katika jamii ya Wameru, unaotumika kwa matambiko, sala na baraka za kijamii.

Askofu Pallangyo: “Tumeomba Mungu Atusamehe Na Atupe Mwanzo Mpya”
Akiongoza sala hizo, Askofu Judah Kundael Pallangyo alisema kuwa Taifa lilipitia kipindi kigumu ambacho kilisababisha kupoteza ndugu na marafiki, hivyo maombi hayo yalikuwa ya kutafuta msamaha wa Mungu na kuomba ukurasa mpya wa upendo na umoja.



“Tunatambua kilichotokea. Nchi ilipita kwenye majaribu makubwa. Ni jukumu letu kumuomba Mungu atusamehe na kutupa nguvu za kujenga upya mshikamano wetu,” alisema.
Ameongeza kuwa kupitia maombi ya wananchi wa Arumeru chini ya Mti wa Mringaringa, Mungu ameisikia Tanzania, na sasa ni wakati wa kujenga nchi bila kuangalia tofauti za kisiasa.
Mbunge Joshua Nasari: “Nitawatumikia Wananchi Wote—Amani Ndio Kipaumbele”
Maombi hayo yaliratibiwa na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Samwel Nasari, ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa wananchi kwa kumchagua kuongoza jimbo hilo.



Akiwahutubia mamia ya wananchi waliohudhuria, Nasari alisisitiza kuwa hatakuwa mbunge wa chama fulani, bali wa wananchi wote:
“Nimeapa kuwatumikia wote bila kujali itikadi. Wananchi wanahitaji maendeleo, si siasa zisizoisha.”
Mbunge huyo aliahidi kusimamia upatikanaji wa:



- Barabara za uhakika zinazopitika muda wote
- Maji safi na salama
- Uunganishaji wa umeme vijijini
- Huduma bora za afya katika hospitali na zahanati
Ameitaka Halmashauri ya ya Wilaya ya Arumeru kuheshimu wananchi na kushirikiana nao kutatua changamoto zao.
Uongozi wa Halmashauri: “Ni Wakati wa Kazi, Sio Siasa”
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Lukas Essaya, aliwahakikishia wananchi kuwa baraza lake litaweka mbele masuala ya maendeleo bila ubaguzi:
“Wananchi wametutuma kufanya kazi, si kukwamisha miradi. Tutashirikiana kikamilifu na Mbunge Nasari kutekeleza ahadi zilizotolewa kipindi cha kampeni.”
Sala za Maridhiano, Mshikamano na Baraka za Mila
Tukio hilo pia limeshuhudia viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali wakiongoza sala za kuombea:

- Maridhiano ya kitaifa
- Mshikamano wa Watanzania
- Hekima kwa viongozi
- Faraja kwa familia zilizoguswa na vurugu


Wazee wa mila wa Washili nao walitoa baraka za kimila, wakisisitiza kulindwa kwa misingi ya amani ambayo imekuwa nguzo ya jamii ya Wameru kwa vizazi vingi.
Wito kwa Taifa: “Tuzidi Kulinda Amani”
Katika tamko la pamoja, viongozi wa dini, wazee wa mila na wanasiasa walitoa wito kwa:
- Serikali
- Vyama vya siasa
- Wananchi wote.



Kutanguliza uzalendo, busara na hekima ili matukio kama ya Oktoba 29 yasijirudie tena.
Hitimisho: Mshikamano Chini ya Mti wa Mringaringa
Kusanyiko hilo lilifungwa kwa sala za baraka chini ya Mti wa Mringaringa, ishara ya umoja na mshikamano wa kipekee kati ya viongozi wa dini, wazee wa mila, viongozi wa kisiasa na jamii kwa ujumla.


MWisho .



