Na Geofrey Stephen . ARUSHA
Desemba 5, 2025
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameiagiza serikali kuanzisha mfumo maalum wa ukusanyaji na uratibu wa tafiti za kilimo ili kuboresha uchambuzi na matumizi ya tafiti hizo, kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao (CROSAT) uliofanyika jijini Arusha, Pinda alisema kuwa mfumo huo utakapotekelezwa kwa ufanisi, utatoa fursa kwa serikali kuwa na taarifa sahihi kutoka kila mkoa. Hii itasaidia kupanga mikakati bora ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima, hususan katika kipindi cha mabadiliko ya tabianchi.


“Mfumo huu utasaidia serikali kubaini kwa urahisi changamoto zinazowakabili wakulima katika kila eneo na kuchukua hatua stahiki. Aidha, utaongeza ajira na kuchangia katika kukuza mchango wa kilimo katika uchumi wa taifa,” alisema Pinda.
Pinda alifafanua kuwa serikali imeendelea kuimarisha sekta ya utafiti nchini kwa kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 40.73 katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), fedha ambazo zimetumika kutengeneza teknolojia mpya 64 za kilimo. Teknolojia hizi zinatoa suluhisho la kuongeza tija, ufanisi, na ustahimilivu wa mazao dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.


“Kwa kuwepo kwa mfumo huu maalum, tafiti zote zitajumuishwa na serikali itakuwa na uwezo wa kuchambua changamoto za wakulima katika maeneo tofauti, hatua itakayosaidia kupanga mikakati inayohitajika,” aliongeza Waziri Mkuu huyo Mstaafu.
Sekta ya Kilimo Yaendelea Kukuwa
Aidha, Pinda alibainisha kuwa juhudi zinazofanywa na serikali katika kukuza sekta ya kilimo zimeiwezesha Tanzania kufikia asilimia 128 ya uzalishaji wa chakula, kiasi kinachozidi mahitaji ya ndani na kuruhusu ziada kuuzwa nje ya nchi.
“Huu ni ushahidi wa mafanikio ya sekta ya kilimo. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba kila mkoa unapata teknolojia inayohitajika ili kuongeza tija na ustahimilivu wa mazao,” alisema Pinda.
Juhudi za Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Pinda pia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) ili kuwafikia vijana wengi zaidi, hasa wale wa vijijini. Lengo ni kuhamasisha mageuzi katika sekta ya kilimo, hatua itakayochochea ukuaji wa kilimo cha kisasa na kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
CROSAT na Ushirikiano wa Wataalamu
Kwa upande wake, Rais na Mwenyekiti wa CROSAT, Profesa Kalunde Sibuga, alieleza kuwa chama hicho kinajivunia kuwa na wanachama 294 kutoka sekta binafsi, taasisi za utafiti, mashirika, na wataalamu wa sayansi za mazao. Profesa Sibuga alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa kilimo na serikali ili kuboresha sekta hiyo, kuongeza ajira, na kuhakikisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.


“Sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa uchumi wa taifa. Ili kufikia malengo ya kisasa ya kilimo, ni lazima tushirikiane kwa karibu na kuhakikisha kwamba teknolojia mpya zinapata matumizi bora na ya haraka.”
Mwisho .


