MBEYA: WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na maafa kwa kutekeleza sera, sheria na miradi ya kimkakati inayolenga kulinda maisha ya wananchi, mali na rasilimali za nchi.
Akizungumza jijini Mbeya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa, Majaliwa alisema Serikali imechukua hatua kadhaa zenye lengo la kuongeza ustahimilivu wa taifa, ikiwemo kuhuisha Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa (2025), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022–2027), na Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa (2022).

Amesema juhudi hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kufikia asilimia 85, hali ambayo imechangia kupunguza madhara ya maafa kwa zaidi ya asilimia 30. Aidha, Serikali imeimarisha mifumo ya tahadhari za mapema kupitia teknolojia za kisasa na Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Majanga.
Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Majaliwa alitaja utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama sehemu ya mikakati endelevu ya kulinda mazingira na vyanzo vya maji, ikiwemo:
Mradi wa Bwawa la Kidunda (Shilingi bilioni 329)
Bwawa la Farkwa (Shilingi bilioni 312)
Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria hadi Simiyu (Shilingi bilioni 440)
Ameeleza kuwa sekta ya kilimo nayo imenufaika kupitia utekelezaji wa mbinu za kilimo himilivu, zikiwemo matumizi ya teknolojia za umwagiliaji, mbegu bora na mifumo ya tahadhari mapema ili kuwasaidia wakulima kupunguza athari za majanga ya asili.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeimarishwa kwa vifaa vya kisasa, teknolojia mpya na mafunzo ya kitaalamu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa uokoaji wakati wa majanga.

Majaliwa ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na serikali kwa kuwekeza kwenye miradi yenye mwelekeo wa ustahimilivu wa majanga, pamoja na kuhakikisha uwekaji wa bima na ufuatiliaji wa miongozo ya usalama wa kitaifa.
Kwa upande wao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Sandra Hakim, wamesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau wote – wakiwemo vijana, viongozi wa jamii na taasisi za kimataifa – katika kuzuia, kujiandaa na kurejesha hali baada ya majanga, ili kujenga taifa lenye ustahimilivu endelevu.