MBEYA: Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mbeya kimeonyesha teknolojia ya kisasa ya mfumo wa Hybrid kwa magari katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea mkoani humo, likionesha namna ubunifu unavyoweza kuchochea maendeleo ya sekta ya usafiri nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwanafunzi Adam Akyoo alisema teknolojia hiyo inalenga kupunguza gharama za uendeshaji wa magari na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati.

“Mfumo wa Hybrid unamwezesha dereva kuendelea na safari hata mafuta yanapokwisha, kwani gari huendeshwa kwa kutumia umeme. Hii ni suluhisho la haraka kwa wamiliki wa magari ya kisasa na njia ya kupunguza utegemezi wa mafuta,” alisema Akyoo.
Amefafanua kuwa mfumo huo unaunganisha mota ya umeme kwenye injini ya gari, ambapo umeme huzalishwa na kusaidia kuendesha gari hata mafuta yanapokosekana, jambo linalosaidia hasa maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa vituo vya mafuta.

“Tumeleta teknolojia hii kama sehemu ya mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia duniani, hasa kwenye sekta ya usafiri ambayo sasa inategemea magari ya umeme,” aliongeza Akyoo.
Kwa upande wake, Ofisa Habari na Uhusiano wa VETA Taifa, David Mpondyo, alisema taasisi hiyo imeongeza nguvu katika kufundisha fani zinazohusiana na teknolojia mpya, hususan magari ya umeme na mfumo wa Hybrid, ili vijana wa Kitanzania wawe tayari kwa mahitaji ya soko la sasa na la baadaye.
“Zamani tulifundisha zaidi magari ya petroli na dizeli, lakini sasa tunapanua wigo hadi kwenye teknolojia za magari ya umeme. Dunia inaelekea huko, na tunataka vijana wetu wawe sehemu ya mabadiliko hayo,” alisema Mpondyo.
Amesema kwa sasa VETA ina zaidi ya vyuo 80 nchi nzima, huku serikali ikiendelea na mpango wa kujenga vyuo 65 vipya katika kila wilaya, ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kupata mafunzo ya ufundi kwa gharama nafuu na hatimaye kujiajiri au kuajiri wengine.
Mpondyo aliongeza kuwa katika baadhi ya vyuo kama VETA Dodoma na VETA Moshi, tayari zimeanzishwa kozi mpya kama ukarabati wa magari ya umeme, uuzaji wa teknolojia bunifu, na welding ya viwango vya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya miradi mikubwa kama EACOP.
“Tunahimiza vijana wachangamkie fursa hizi. Elimu ya ufundi si kwa waliokosa, bali ni msingi wa maisha ya kisasa. Hata kama hujafika chuoni, tembelea banda letu hapa maonyesho ujifunze na ujue namna ya kujiunga,” alisema.