TANNA Yaitaka Serikali Kutimiza Ahadi ya Muundo Mpya wa Wauguzi na Wakunga Julai 2025

Geofrey Stephen
2 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha

Arusha – Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA) kimeiomba serikali kutimiza kilio cha muda mrefu cha kada hiyo kwa kuhakikisha inakamilisha muundo mpya wa maendeleo ya utumishi, unaotarajiwa kuanza rasmi Julai 2025.

Habari Picha 3058

Akizungumza jijini Arusha mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati tendaji, Rais wa TANNA, Dkt. Ezekiel Mbao, alisema malalamiko ya muda mrefu kuhusu muundo wa kada hiyo yamekuwa yakijirudia tangu mwaka 2013.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wauguzi juu ya muundo wa maendeleo ya utumishi wa kada yetu. Taarifa tulizowahi kuwasilisha serikalini mara kwa mara bado hazijapatiwa majibu stahiki. Hali hii imezua taharuki kwa wauguzi na wakunga kote nchini, jambo linalodhoofisha imani yao kwa ahadi zinazotolewa na serikali,” alisema Dkt. Mbao.

Habari Picha 3062

Kwa upande Makamu wa Rais  wa TANNA, Pendo Shayo, alisisitiza kuwa kuchelewa kwa utekelezaji wa ahadi hizo kumeathiri ari ya watumishi wengi, hasa wale walioboresha taaluma zao bila kupata nyongeza za madaraja na mishahara.

Habari Picha 3060

“Wengi wetu tumebaki pale pale kwa muda mrefu, licha ya kujiongezea ujuzi kitaaluma. Hii ni kinyume na taratibu za kazi. Tunaiomba serikali isikie kilio chetu ili tufanye kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Shayo.

Aidha, Katibu Mkuu wa TANNA, Chacha John, alisisitiza umuhimu wa serikali kutimiza ahadi hiyo akibainisha ukubwa wa mchango wa wauguzi na wakunga katika jamii.

“Wauguzi na wakunga ndio wa kwanza kumpokea mtoto anapozaliwa na pia wanakuwa wa kwanza kumhudumia mtu anapofariki. Wanabeba jukumu kubwa sana katika sekta ya afya, hivyo ni haki yao changamoto zao kushughulikiwa kwa haraka,” alisema John.

Habari Picha 3061

Kwa mujibu wa viongozi wa TANNA, chama hicho kitaendelea kufuatilia suala hili kwa karibu hadi pale serikali itakapotimiza ahadi yake ya muda.

 

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment