Wanafunzi Wathibitisha Uchaguzi wa Amani kwa Matemebezi”

Geofrey Stephen
3 Min Read

Makala Maalum

Jua lilikuwa linawaka taratibu juu ya mlima Meru, likiangaza mitaa ya jiji la Arusha kwa mng’aro wa asubuhi tulivu. Katika barabara zinazoelekea ofisi ya Mkuu wa Mkoa, sauti za watoto zilisikika zikishindana na upepo wa Septemba—nyimbo, vifijo na kauli mbiu zilizobeba ujumbe mmoja: amani.

Hawakuwa wanasiasa, wala viongozi wa dini. Walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Green Valley, wakiwa kwenye matembezi ya amani kuelekea kusherehekea miaka 25 ya shule yao. Waliandamana wakiwa wamevalia sare safi za shule, mabango mikononi yakiwa yameandikwa maneno kama “Amani ni Msingi wa Elimu” na “Bila Amani Hatuna Mustakabali”.

Habari Picha 3026
Habari Picha 3027

Wakati kundi hilo dogo la wanafunzi liliposimama mbele ya jengo kubwa la ofisi ya Mkuu wa Mkoa, walipokelewa kwa joto na mwenyeji wao, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla. Uso wake ulijaa tabasamu, kana kwamba alitambua kuwa ujumbe wa watoto hao ulikuwa wa thamani zaidi kuliko maelfu ya hotuba za kisiasa.

Kwa sauti yenye uzito lakini yenye ukaribu, Makalla aliwageukia wanafunzi na wananchi waliokusanyika:

“Nataka niwahakikishie kuwa mtasoma kwa amani, mtaishi kwa amani na uchaguzi utafanyika kwa amani. Kuanzia sasa, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi, nchi yetu itaendelea kuwa na utulivu. Nawapongeza kwa kuadhimisha miaka 25 kwa kuhamasisha amani. Mkasome kwa amani, na nchi yetu itaendelea kuwa na amani.”

Maneno hayo yalipokelewa kwa makofi na nyimbo. Ilikuwa kana kwamba kila mtu aliyekuwepo alipata pumzi mpya ya matumaini.

Wanafunzi, kwa upande wao, walizungumza kwa dhati isiyo na shaka. Walieleza kwamba wamesafiri barabarani kwa lengo moja: kuwakumbusha Watanzania wote kuwa amani ndio nguzo ya elimu na maendeleo. Bila utulivu, walisisitiza, masomo yao yangevurugika na mustakabali wao kama kizazi kijacho ungewekwa rehani.

Habari Picha 3030

 

Habari Picha 3028

Katika macho ya wananchi waliokuwepo, ujumbe huo uliotolewa na watoto wadogo ulikuwa wa kugusa zaidi kuliko maneno ya kampeni yoyote. Amani, walionyesha, haipaswi kuachwa mikononi mwa wanasiasa pekee—ni jukumu la kila mmoja, kuanzia mwanafunzi mdogo hadi kiongozi mkuu wa nchi.

Siku hiyo haikubaki tu kama kumbukumbu ya maadhimisho ya shule; iligeuka kuwa somo kubwa la kijamii. Sherehe za Green Valley zilifungua ukurasa mpya wa fikra, zikimkumbusha kila mmoja kuwa uchaguzi huja na kuondoka, lakini thamani ya amani haiwezi kufutika.

Habari Picha 3031

Arusha ilishuhudia siyo tu shamrashamra za watoto, bali pia sauti ya kizazi kipya kikitoa wito wa amani kwa taifa zima.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment