Na Geofrey Stephen Karatu .
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, amekanusha madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba alihusika au alitoa amri ya kufyekwa kwa mazao katika eneo lenye mgogoro la Kijiji cha Oldeani, Kata ya Endabash, wilayani Karatu.
Madai hayo yanahusisha uharibifu wa takribani hekari 27 za mazao, yakiwemo migomba, miwa na mahindi. Baadhi ya wananchi pia wamedai kuwa nyumba zao zilichomwa moto wakati wa zoezi hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Karanga amesema ofisi yake haikutoa agizo la kufyeka mazao hayo, akieleza kuwa taarifa za tukio hilo aliziona kupitia mitandao ya kijamii.

“Ofisi yangu haikutoa agizo la kufyeka mazao hayo. Mimi mwenyewe niliona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii,” amesema Karanga.
Mgogoro wa Oldeani waanza mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mgogoro wa eneo hilo si wa hivi karibuni, bali umedumu kwa miaka kadhaa tangu mwaka 2017, wakati ambapo yeye hakuwa bado Mkuu wa Wilaya ya Karatu.
Karanga amesema tangu kuanza kwa mgogoro huo, wananchi waliokuwa wakiishi au kutumia eneo hilo wamekuwa wakielekezwa mara kadhaa kuondoka, huku eneo hilo likidaiwa kumilikiwa na mwekezaji wa Kongoni Estate.
Amesema viongozi wa wilaya pamoja na wataalamu wa kilimo waliwahi kufika katika eneo hilo katika hatua mbalimbali za kutafuta suluhu na kutoa maelekezo kwa wananchi kuondoka.
Kwa mujibu wa Karanga, baadhi ya hoja zilizokuwa zikihusishwa na mgogoro huo ni matumizi ya eneo pamoja na masuala yanayohusu vyanzo vya maji.
Mwekezaji apeleka mgogoro mahakamani
Mkuu huyo wa Wilaya amesema baada ya hatua mbalimbali za kiutawala kushindwa kumaliza mgogoro huo, mwekezaji aliamua kufikisha suala hilo mahakamani.
Amesema wananchi walipewa notisi za kuondoka kupitia court broker, hatua aliyosema ilikuwa sehemu ya mchakato wa kisheria.
Hata hivyo, Karanga amesema baada ya yeye kuingia katika suala hilo, alikutana na pande zote na kusisitiza wananchi wapewe muda wa kutosha ili waweze kuondoka kwa amani.
“Nilipokutana na pande zote, msisitizo wangu ulikuwa wananchi wapewe muda wa kutosha ili waondoke kwa amani,” amesema.
DC Karatu akanusha madai ya viboko na lockup.
Karanga pia amekanusha tuhuma nyingine zinazomhusisha na kukamatwa kwa wananchi waliokuwa wakilalamikia mgogoro huo.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai kupitia mitandao ya kijamii kwamba waliwekwa lokapu na kwamba walikuwa wakipigwa viboko vitatu kila asubuhi kwa maagizo ya Mkuu huyo wa Wilaya.
Hata hivyo, Karanga ameyakana madai hayo, akisema ofisi yake haikutoa amri hiyo na kwamba Jeshi la Polisi halikufanya tukio hilo kwa maelekezo yake.
Amewataka wananchi wenye malalamiko kuhusu migogoro ya ardhi kutumia taratibu na vyombo vinavyotambulika kisheria.
Wananchi wadai mazao na nyumba zao kuharibiwa
Awali, wakazi watatu wa eneo hilo waliosikika kupitia mitandao ya kijamii walimtuhumu Karanga kuhusika na agizo la kufyekwa kwa mazao yao katika eneo lenye ukubwa wa takribani hekari 27.

Wananchi hao walidai kuwa mazao yaliyoharibiwa yalikuwa ni pamoja na migomba, miwa na mahindi.
Pia walidai kuwa baadhi ya nyumba zao zilichomwa moto wakati wa zoezi hilo.
Mmoja wa walalamikaji alidai kuwa kiasi cha Sh5 milioni kilichokuwa ndani ya nyumba yake kilipotea, pamoja na vitu vingine vya thamani.
Wananchi hao walisema uharibifu wa mazao umeathiri maisha yao kwa kuwa mazao hayo yalikuwa chanzo cha chakula na kipato kwa familia zao.
Hata hivyo, madai hayo ni ya wananchi waliosikika kupitia mitandao ya kijamii na hayajathibitishwa kwa kujitegemea, huku Mkuu wa Wilaya akiyakanusha na kusema ofisi yake haikutoa amri ya kufanyika kwa uharibifu huo.
DC awataka wananchi kuheshimu umiliki wa ardhi
Karanga amewataka wananchi kuheshimu maeneo yanayomilikiwa na watu wengine na kuacha kuingia au kutumia maeneo bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema migogoro ya ardhi inapaswa kushughulikiwa kupitia mamlaka na vyombo vya sheria vinavyotambulika badala ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Pia amewataka wananchi wanaohusika katika migogoro ya ardhi kufuata maamuzi na taratibu zinazotolewa na vyombo vya sheria.
Awasihi waandishi wa habari kusikiliza pande zote.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchapisha taarifa zinazohusu migogoro ya ardhi.
Amesisitiza umuhimu wa kusikiliza pande zote zinazohusika ili kuhakikisha taarifa zinazofikishwa kwa umma zinakuwa na usawa na kuakisi maelezo ya kila upande.
Mgogoro wa eneo la Oldeani umeendelea kuzua mjadala, huku wananchi wakitoa madai mbalimbali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Serikali ya Wilaya ya Karatu imesisitiza kuwa mgogoro huo una historia ya muda mrefu, ulianza tangu mwaka 2017 na umewahi kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hadi sasa, madai kuhusu uharibifu wa mazao, uchomaji wa nyumba na upotevu wa mali yanahitaji uthibitisho zaidi kutoka kwa mamlaka husika na uchunguzi wa kina wa pande zote zinazohusika.
Mwisho.
