Na Geofrey Stephen . ARUSHA:
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeanza kuimarisha mifumo ya usalama wa nyuklia nchini ili kuhakikisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zinafanyika katika mazingira salama, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi mbalimbali katika kukabiliana na vitisho vinavyoweza kujitokeza.
Mkurugenzi wa TAEC, Profesa Najat Mohammed, amesema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tano ya kujenga uwezo kwa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, vyombo vya usalama, Mamlaka za Forodha na Uhamiaji pamoja na wasimamizi wa viwanja vya michezo.

Profesa Najat amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uwezo wa taasisi hizo katika kutekeleza hatua za usalama wa nyuklia wakati wa matukio makubwa ya umma, akieleza kuwa Tanzania imeanza maandalizi ya kina kutokana na ukubwa na hadhi ya AFCON 2027.
AFCON 2027 kuhitaji maandalizi maalumu ya kiusalama.
Kwa mujibu wa Profesa Najat, mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia wachezaji, mashabiki, waandishi wa habari na wananchi kutoka sehemu mbalimbali duniani, jambo litakalofanya Tanzania kuwa chini ya uangalizi mkubwa wa kimataifa.
Kutokana na hali hiyo, amesema kunahitajika mipango ya usalama iliyopangiliwa na kuratibiwa kwa kuzingatia tathmini ya vitisho na hatari zinazoweza kujitokeza.

Alisisitiza kuwa usalama wa nyuklia katika tukio kubwa la umma hauwezi kusimamiwa na taasisi moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka za udhibiti, waendeshaji wa miundombinu muhimu na wadau wengine.
TAEC yaimarisha uwezo wa kugundua mionzi.
Profesa Najat amesema warsha hiyo ni jukwaa muhimu la kuimarisha uratibu wa taasisi zinazohusika, kuweka wazi majukumu ya kila mmoja na kujenga uwezo wa pamoja katika kuhakikisha usalama wakati wa matukio makubwa.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha uwezo wa kuzuia, kubaini na kukabiliana na matukio yanayohusiana na usalama wa nyuklia..

Hatua hizo ni pamoja na kuweka vifaa vya kugundua mionzi katika baadhi ya vituo vya mipaka na maeneo muhimu ya kimkakati.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa maofisa walio mstari wa mbele ili kuwaongezea ujuzi wa kitaalamu, sambamba na kuimarisha uratibu wa mifumo ya kitaifa ya maandalizi na mwitikio wa dharura.
Tathmini ya vitisho na mazoezi ya uwandani
Profesa Najat amesema matukio makubwa kama AFCON 2027 yana mahitaji ya kiusalama yanayohitaji maandalizi maalumu, yakiwemo kufanya tathmini ya vitisho na hatari,
kubadilishana taarifa kwa wakati na kuweka mfumo madhubuti wa amri na udhibiti.
Pia amesema ni muhimu kuweka vifaa vya kugundua mionzi katika maeneo yanayofaa ili kusaidia kubaini mapema vitisho vinavyoweza kujitokeza.
Katika warsha hiyo ya siku tano, washiriki wanapata mafunzo ya kinadharia na vitendo kuhusu hatua za kuzuia vitisho, utambuzi wa mionzi, tathmini ya tahadhari, taratibu za upekuzi na mwitikio ulioratibiwa.
Washiriki pia watashiriki katika mazoezi ya uwandani yatakayowapa fursa ya kutumia kwa vitendo ujuzi wanaoupata, pamoja na kutathmini uwezo wa Tanzania wa kujiandaa na kukabiliana na changamoto za usalama wa nyuklia wakati wa AFCON 2027.
IAEA yaipongeza Tanzania.
Naye Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Lacina Saro, ameipongeza Tanzania kwa kuanza mapema kuimarisha maandalizi ya usalama wa nyuklia katika matukio makubwa ya umma, ikiwemo AFCON 2027.
Saro amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 ni jambo la kujivunia, lakini pia linaambatana na wajibu mkubwa wa kuhakikisha usalama wa mashindano hayo.
“Uchaguzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 ni jambo la kujivunia, lakini pia unaambatana na wajibu. Hivyo, mpango wa usalama wa nyuklia wa kiwango hiki unapaswa kuandaliwa mapema, kufanyiwa majaribio kwa kina na kutekelezwa kwa ufanisi na timu za kitaifa zilizopewa mafunzo,” alisema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, IAEA inaendelea kusaidia nchi wanachama kuimarisha miundombinu yao ya kitaifa ya usalama wa nyuklia kupitia miongozo, mafunzo na msaada wa kiufundi.
“Tuko hapa kufanya kazi pamoja nanyi na kuunga mkono Tanzania katika kujenga uwezo wa usalama wa nyuklia ambao mnaweza kuutegemea wakati wa AFCON 2027 na hata baada ya mashindano hayo,” alisema Saro.
Tanzania yaweka nguvu kwenye wataalamu na vifaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Dk. Remigius Kamala, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu zitakazokuwa wenyeji wa AFCON 2027 ambazo zimeanza maandalizi ya usalama wa nyuklia na mionzi.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika wataalamu na vifaa kwa ajili ya kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira salama.

Dk. Kamala amesema Tanzania ina uwezo mkubwa katika eneo la teknolojia ya nyuklia na mionzi, ikiwemo kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kutumia teknolojia hiyo pamoja na vifaa vinavyoweza kusaidia kubaini na kukabiliana na vitisho vya mionzi wakati wa matukio makubwa ya umma.
Amesema uwezo huo unaipa Tanzania nafasi nzuri ya kujiandaa mapema na kuhakikisha mifumo ya usalama wa nyuklia inafanya kazi kwa ufanisi kabla na wakati wa mashindano hayo.
Dk. Kamala pia amezishukuru IAEA, wataalamu wa kimataifa, China pamoja na washiriki na taasisi mbalimbali kwa ushirikiano wao katika warsha hiyo.
Amewataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kushiriki katika majadiliano na mazoezi ya vitendo ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kukabiliana na changamoto za usalama wa nyuklia.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, huku maandalizi ya kiusalama yakilenga kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa usalama na mafanikio.

Mwisho…
