Na Geofrey Stephen Karatu .
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dkt. Lameck Karanga, ametembelea Shule ya Sekondari Kilimamoja na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa shuleni hapo kwa ufadhili wa andBeyond Ngorongoro Crater Lodge kwa kushirikiana na Wild Impact.
Miradi hiyo inajumuisha Jengo la Utawala, Maabara ya Kompyuta, vyoo vya shule pamoja na mabweni mawili ya wanafunzi, ikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.


Katika hafla hiyo, Mkuu wa Shule, Monica Alex Mboya, ameeleza umuhimu wa miradi hiyo katika kuboresha mazingira ya shule na kusaidia wanafunzi kupata huduma bora za elimu.
Kwa upande wa Wild Impact, mwakilishi wake McDonald Mlemwa, amesisitiza dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na jamii katika kuunga mkono maendeleo ya elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia.


Naye mwakilishi wa andBeyond Ngorongoro Crater Lodge, Dkt. Charles, ameeleza dhamira ya taasisi hiyo katika kushirikiana na jamii zinazozunguka maeneo ya utalii kupitia uwekezaji katika miradi ya kijamii, hususan elimu.
Aidha, kupitia ufadhili huo, shule imepokea kompyuta 25 kwa ajili ya mafunzo ya TEHAMA pamoja na vitabu 800 kwa ajili ya maktaba mpya, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa vitendea kazi na kukuza utamaduni wa kusoma miongoni mwa wanafunzi.


Mhe. Dkt. Lameck Karanga amepongeza andBeyond Ngorongoro Crater Lodge na Wild Impact kwa mchango wao katika kuboresha miundombinu ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza na kutumia vizuri miradi hiyo ili iwe na manufaa kwa wanafunzi na jamii kwa muda mrefu.



MWISHO…
