“FEDHA ZA WANANCHI ZISIPOTELE” — AITAKA TAKUKURU NA SERIKALI KUFANYA KAZI KWA PAMOJA.

Geofrey Steven
6 Min Read

Na Geofrey Stephen

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutotumia ufuatiliaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kama sababu ya kuchelewesha miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa fedha za wananchi lazima zilindwe na zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Makalla alitoa kauli hiyo wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo Mkoa wa Arusha, iliyowakutanisha viongozi na watendaji wa Serikali, halmashauri, taasisi za udhibiti, vyombo vya sheria pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 

Habari Picha 19878

Alisema mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la TAKUKURU pekee, bali linahitaji ushirikiano wa Serikali, vyombo vya sheria, taasisi za udhibiti, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.

“Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu. Tutimize wajibu wetu,” alisema Makalla.
TAKUKURU ISITUMIKE KAMA KISINGIZIO
Makalla alisema ufuatiliaji unaofanywa na TAKUKURU katika miradi ya maendeleo unalenga kuhakikisha fedha za umma zinalindwa na miradi inatekelezwa kwa usahihi, hivyo haupaswi kutumiwa kama sababu ya kusimamisha au kuchelewesha utekelezaji.

“Tusitumie TAKUKURU kama chaka la kuchelewesha miradi. TAKUKURU inapofuatilia mradi, lengo ni kuhakikisha mambo yanaenda vizuri na hakuna fedha za wananchi zinazopotea,” alisema.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za udhibiti ni muhimu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

AONYA KUCHEPUSHA FEDHA ZA MIRADI.

Makalla pia alisisitiza kuwa fedha zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kutumika kwa kazi zilizokusudiwa.

Alionya viongozi na watendaji wanaosimamia fedha za umma dhidi ya kuzichepusha, akisema fedha hizo zinapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Habari Picha 19883

“Fedha nyingi zinazotolewa na Serikali na kutajwa katika bajeti zinapaswa kufika mkoani na kutumika kwa kazi iliyokusudiwa. Hakuna kutengeneza namna yoyote ya kuzichepusha,” alisema.

Alisema uadilifu katika usimamizi wa fedha za umma unapaswa kuambatana na uzingatiaji wa sheria, haki na uwajibikaji.
Aidha, aliwataka watendaji wanaohusika na ukaguzi, ufuatiliaji na usimamizi wa fedha za umma kulinda uhuru wao wa kitaaluma na kuepuka kupokea zawadi, huduma au upendeleo kutoka kwa watu wanaowasimamia au kuwafanyia ukaguzi.

ATAKA TAARIFA ZA MIRADI KUTOLEWA KWA WAKATI.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali inahitaji taarifa sahihi na za wakati kuhusu utekelezaji wa miradi ili changamoto ziweze kubainika mapema na kuchukuliwa hatua kabla hazijasababisha hasara.

Alisema utafiti, uchunguzi, ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ni muhimu katika kuisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi.
“Changamoto za miradi zinapaswa kubainika mapema na kushughulikiwa kabla hazijasababisha hasara kwa Serikali na wananchi,” alisema.

Habari Picha 19879

NGUVILLA: UTAWALA BORA NI LAZIMA.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvilla, alisema viongozi mkoani humo wana wajibu wa kuimarisha utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Nguvilla alisema mapambano dhidi ya rushwa katika utekelezaji wa miradi yanapaswa kupewa kipaumbele, sambamba na kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa wakati na rasilimali za umma zinasimamiwa kwa maslahi ya wananchi.

TAKUKURU YAFUATILIA MIRADI 164 YENYE THAMANI YA SH469 BILIONI.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, alisema taasisi hiyo imefuatilia miradi 164 yenye thamani ya Sh469 bilioni, ambapo miradi 109 ilibainika kuwa na kasoro zilizohitaji hatua za ufuatiliaji na marekebisho.
Alisema hatua hizo zinalenga kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa na wananchi wanapata thamani halisi ya fedha zilizotengwa.

Kwa mujibu wa Ngailo, ukosefu wa fedha, ucheleweshaji wa utekelezaji wa baadhi ya miradi na ushiriki mdogo wa wadau ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri utekelezaji wa miradi kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Habari Picha 19882

“Ucheleweshaji wa baadhi ya miradi, pamoja na ushiriki mdogo wa wadau, haya yote kwa pamoja yanafanya miradi hii kutekelezwa nje ya muda au ikiwa na mapungufu,” alisema Ngailo.

Alisema warsha hiyo imelenga kuwaunganisha wadau ili kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo, kuongeza ushiriki wa jamii katika ufuatiliaji wa miradi na kuhakikisha rasilimali zinazotengwa zinatumika kwa ufanisi.

KUZUIA RUSHWA NI JUKUMU LA KILA MMOJA’

Ngailo alisema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na Serikali inapata thamani ya fedha inayowekeza katika miradi ya maendeleo.

“Tunategemea kwamba mikakati itakayowekwa itasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, lakini mwisho itasaidia wote kushiriki katika kusimamia miradi hii, ili tuweze kupata thamani ya fedha ambayo imekusudiwa katika uanzishaji wa miradi husika,” alisema.

Habari Picha 19884

Alisisitiza kuwa kila mdau mwenye dhamana ya kusimamia, kutekeleza au kufuatilia miradi ana wajibu wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia malengo, thamani ya fedha na muda uliopangwa.
“Kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja,” alisema.

MAKALLA: TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU.

Akihitimisha, Makalla alisema Serikali ya Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana na TAKUKURU pamoja na taasisi nyingine za udhibiti kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mujibu wa sheria, viwango na muda uliopangwa.

“TAKUKURU na taasisi zote za Serikali pamoja na watendaji tutaenda kwa pamoja kwa sababu sisi wote tunategemeana. Lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza mapambano ya rushwa, tunaongeza uwajibikaji na kuhakikisha miradi yetu yote inatekelezwa kwa ufanisi,” alisema.

Habari Picha 19886
Habari Picha 19885

Alisema mafanikio ya warsha hiyo hayatapimwa kwa mijadala iliyofanyika pekee, bali kwa utekelezaji wa maazimio na hatua zitakazochukuliwa na kila mdau.
“Tunataka TAKUKURU, Serikali na taasisi zote tufanye kazi kwa pamoja. Tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia kuharakisha maendeleo na kulinda fedha za wananchi,” alisema Makalla.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment