Hai, Kilimanjaro –
Viongozi wa ngazi zote kuanzia vitongoji, vijiji, kata hadi wilaya katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro,
wametakiwa kuimarisha juhudi za kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwalinda vijana, ambao ni nguvu kazi ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Vijana wa Taasisi ya Kiislamu ya Istiqama, Ally Abdallah, wakati wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa taasisi hiyo uliofanyika katika Msikiti wa Gezaulole, Bomang’ombe, Wilaya ya Hai.
Mkutano huo uliwakutanisha waumini wa dini ya Kiislamu, Masheikh kutoka mikoa mbalimbali na viongozi mbalimbali kwa lengo la kujadili maendeleo ya taasisi, uchumi na kuombea amani ya taifa.

Akizungumza Agosti 2, 2026, Ally alisema matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa tishio kwa jamii, hususan kwa vijana, na kwamba viongozi wanapaswa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo.
“Tunawaomba viongozi katika maeneo yao kuzuia kuingia na kusambazwa kwa dawa hizi. Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa, hivyo wakiharibika, taifa nalo linaathirika. Hali ni mbaya mitaani,” alisema.
Alieleza kuwa katika maeneo mengi, ikiwemo Bomang’ombe, matumizi ya bangi hufanyika hata hadharani, jambo linaloonyesha ukubwa wa changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Ally, matumizi ya dawa za kulevya huongeza uwezekano wa vijana kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama ukabaji, wizi, ubakaji na vitendo vingine vya ukatili vinavyohatarisha usalama wa jamii.
Aliitaka Serikali pamoja na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa karibu kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya inadhibitiwa, akisisitiza kuwa kinga ndiyo njia bora ya kulinda kizazi cha sasa na cha baadaye.
Wazazi Watakiwa Kutenga Muda kwa Watoto
Kwa upande wake, Kiongozi wa Taasisi ya Istiqama Mkoa wa Kilimanjaro, Kileo Bakari, aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuwapa malezi bora na kuwajengea maadili mema.
Alisema wengi wamejikita katika shughuli za kutafuta kipato na kusahau umuhimu wa kutumia muda na watoto wao.
“Mzazi anatoka nyumbani mapema asubuhi na kurudi usiku. Mtoto huyo anapata muda gani wa kuzungumza na mzazi wake? Tunawaomba wazazi wapange ratiba ya kukaa na watoto wao kwa sababu wana mambo mengi ya kuwashirikisha,” alisema.
Istiqama Yaendelea Kuimarisha Maendeleo na Maadili.

Awali, Fakihi Mkuu wa Taasisi ya Istiqama Taifa alisema taasisi hiyo ilisajiliwa mwaka 2013 na imekuwa ikiendesha mikutano mikuu ya kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema pamoja na kukuza Uislamu nchini, taasisi hiyo inalenga kuimarisha miradi ya maendeleo ya kiuchumi, kusimamia maadili ya jamii na kuhamasisha umuhimu wa kudumisha amani nchini.
Alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuilinda.
— Mwisho —
