Na Mwanishi wa A24tv.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameipongeza Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa ushirikiano wake na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI/TaCRI) baada ya kutembelea shamba la kahawa wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 33 Kitaifa (Nanenane) 2026 katika viwanja vya John Malechela Nzuguni, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alijionea mafanikio ya tafiti na teknolojia mbalimbali za kisasa za uzalishaji wa miche bora(Compact) na mbinu zinazolenga kuongeza tija, ubora wa kahawa na kipato cha wakulima. Aidha, ameeleza kufurahishwa kwa kuona kahawa inastawi mkoani Dodoma, akisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa zao hilo linaendelea kustawi katika maeneo mapya na kuufanya mkoa huo kuwa na fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na uchumi wa kahawa.

Mhe. Dkt. Nchemba amezitaka TCB, TARI/TaCRI kuendelea kuimarisha tafiti, ubunifu na utoaji wa huduma kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Maonesho hayo yataendelea hadi Agosti 8,2026 kitaifa katika viwanja vya John Malechela Nzuguni, jijini Dodoma, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Tambua Soko, Zalisha kwa Tija Kutekeleza Dira 2050.”


Mwisho.
