Na Mwandishi wa A24tv.
Hai. Zaidi ya vijana 200 kutoka Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wameanza kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali yenye lengo la kuwawezesha kujiajiri na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia Julai 23 hadi Julai 25, 2026 katika Kilimanjaro Modern Open School iliyopo Bomang’ombe. Yanaendeshwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Chuo cha Elimu kwa Wote kutoka Dar es Salaam, huku yakiratibiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana na wajasiriamali wadogo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Julai 23, 2026, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Saravai Izina, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia vijana kujikwamua kutoka kwenye utegemezi kwa kuwapa maarifa na ujuzi wa kujitegemea kiuchumi na kijamii.
“Taasisi yetu inatoa mafunzo ya ujasiriamali yanayohusisha utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama sabuni, mishumaa, batiki na keki. Tunaamini kupitia mafunzo haya vijana watajenga msingi imara wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo bila kutegemea ajira za Serikali pekee,” alisema Izina.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kukabiliana na changamoto za maisha kwa kutumia ujuzi watakaoupata, huku akiwataka kuyatumia kwa vitendo kwa kuanzisha miradi midogo ya ujasiriamali.
Izina pia alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, kwa kuona umuhimu wa kuwaunganisha vijana na wajasiriamali ili wapate mafunzo hayo.
“Tunampongeza kwa kutuleta hapa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana na wajasiriamali. Hii ni hatua muhimu katika kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na ni mfano unaopaswa kuigwa na viongozi wengine,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, alisema kuwa pamoja na Serikali kuendelea kutoa ajira katika sekta mbalimbali, nafasi hizo haziwezi kukidhi mahitaji ya vijana wote.
“Ajira za Serikali hazitoshi. Kupitia mafunzo haya, vijana watapata maarifa na ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali zitakazowawezesha kujipatia kipato na kujiajiri,” alisema Rutaraka.

Aliwataka vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Halima Salimu kutoka Bomang’ombe, alimshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Muungano kwa kusimamia mafunzo hayo na kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ujasiriamali.
Aidha, alisema Rutaraka ametoa msaada wa shilingi 700,000 kwa ajili ya kuwezesha washiriki kupata vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo.
“Tunampongeza sana kwa moyo wake wa kuwainua vijana. Tunaamini mafunzo haya yatatusaidia kujiajiri na kuboresha maisha yetu,” alisema Halima.
Aliwashauri vijana waliopata mafunzo hayo kuyatumia kwa vitendo kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo badala ya kusubiri ajira za Serikali, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi na kuongeza kipato.


Washiriki wengine walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya wa kupanga maisha yao kupitia ujasiriamali na kuomba yaendelee kutolewa kwa vijana wengi zaidi, hasa wale wanaohitimu masomo na kukosa fursa za ajira.
Mwisho.

