Na Geofrwey Stephen Meru
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwl. Zainabu Juma Makwinya, leo Julai 11, 2026, amepokea Mwenge wa Uhuru 2026 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Seleman Hamis Msumi, katika hafla iliyofanyika eneo la Barabara Mpya Peace Point.
Akizungumza mara baada ya kupokea Mwenge huo, Mwl. Makwinya amesema Mwenge wa Uhuru 2026 utakimbizwa umbali wa kilomita 65.85 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru, huku ukitembelea miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.09.


Amesema miradi hiyo inatekelezwa katika sekta za elimu, afya, maji, mazingira, uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha utoaji wa huduma na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Kwa mujibu wa Mwl. Makwinya, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Ng’onda, ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Amsha wenye thamani ya shilingi milioni 75.
Pia ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Barabara ya Tengeru–Nambala yenye urefu wa kilomita 3.8 katika Kata ya Akheri, unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5.
Katika sekta ya afya, Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya msingi katika mradi wa ujenzi wa Jengo la Radiolojia pamoja na njia za watembea kwa miguu katika Hospitali ya Wilaya ya Meru, mradi unaogharimu shilingi milioni 315.5.
Vilevile, Mwenge huo utatembelea Mradi wa Maji wa Kata ya Kikwe wenye thamani ya shilingi bilioni 3, pamoja na mradi wa uwekezaji wa sekta binafsi wa ujenzi wa jengo la biashara la TYPHA Mall lililopo Leganga, Kata ya Usa River, unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.
Katika eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mwenge wa Uhuru utatembelea mradi wa Kikundi cha Vijana Uchumi Youth Group wenye thamani ya shilingi milioni 101.9. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 50 ni mkopo usio na riba uliotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, huku shilingi milioni 51.9 zikiwa ni mtaji wa kikundi hicho.


Mbali na kukagua miradi ya maendeleo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa atatembelea na kutoa elimu kuhusu masuala ya lishe, mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, malaria na VVU/UKIMWI, sambamba na kuendelea kuhamasisha wananchi kutekeleza ujumbe na maadili ya Mwenge wa Uhuru.
Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 unabeba kaulimbiu isemayo, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane Kuijenga,” ikiwa ni wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana katika kulinda amani, umoja na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Mwwisho…

