MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI MKUBWA WA UPASUAJI WA DHARURA JIJINI ARUSHA.

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Geofrey Stephen

Arusha,

Julai 9, 2026 – Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa jengo la upasuaji wa dharura katika Kituo cha Afya Moivaro, kilichopo Jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya na kuzipeleka karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mwang’onda alisema ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali unaolenga kuboresha huduma za afya nchini, hususan kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura.

Habari Picha 19237
Habari Picha 19238

Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za msingi karibu na maeneo wanayoishi.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza dhamira yake ya dhati ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuhakikisha huduma za msingi zinapatikana katika kata mbalimbali nchini. Niwaombe wananchi wa Arusha waendelee kumuunga mkono ili aendelee kutekeleza mipango ya maendeleo. Aidha, Mheshimiwa Rais anasisitiza amani na utulivu, ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu,” alisema Mwang’onda.

Habari Picha 19239
Habari Picha 19240

Mradi huo una thamani ya shilingi milioni 376.7 na umegharimiwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha. Unatarajiwa kuboresha huduma za upasuaji wa dharura kwa wakazi wa eneo la Moivaro na maeneo jirani, kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za ngazi za juu, pamoja na kuchangia kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na changamoto za uzazi.

Uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi huo ni sehemu ya shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, ambazo pamoja na kuhamasisha uzalendo, umoja na amani, pia hukagua, kuzindua na kuhamasisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayowanufaisha wananchi nchini.

Habari Picha 19241
Habari Picha 19242

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment