Na Geofrey Stephen Arusha.
Serikali imeanza rasmi utoaji wa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 200 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kuanzisha na kukuza biashara, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo Alhamisi, Julai 9, 2026, mkoani Arusha, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alikabidhi hundi ya mfano kwa kikundi cha Umalita Arusha ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kwa utoaji wa mikopo hiyo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Nanauka alisema Serikali imejipanga kuhakikisha fedha za mfuko huo zinawafikia vijana wenye miradi yenye tija ili kuwawezesha kujiajiri, kuajiri wengine na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
“Mafanikio ya programu hii hayatapimwa kwa kiwango cha fedha kilichotolewa, bali kwa matokeo yatakayopatikana. Tunataka kuona biashara zenye tija, ongezeko la ajira, mapato ya wananchi na ukuaji wa kampuni zinazoendeshwa na vijana,” alisema Nanauka.
Alisema Serikali inatarajia mikopo hiyo itakuwa chachu ya kuinua uwezo wa vijana kiuchumi kwa kuwawezesha kuanzisha na kupanua biashara zenye tija, huku akiwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kufanikisha azma ya mfuko huo.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Meru, Haika Mawalla, alisema benki hiyo imejipanga kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji.
Alisema pamoja na kutoa mikopo, CRDB itaendelea kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, uendeshaji wa biashara na matumizi sahihi ya mikopo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinaleta matokeo chanya kwa wanufaika.


“Tunaamini mchanganyiko wa mtaji, maarifa na nidhamu ya fedha ndiyo msingi wa mafanikio ya biashara na ujasiriamali endelevu. Tunawasihi vijana kuitumia fursa hii kwa ubunifu na uwajibikaji ili mikopo hii iwe chachu ya kuongeza uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi,” alisema Mawalla.
Aliongeza kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha programu hiyo inawafikia vijana wengi zaidi nchini, huku ikiendelea kutoa elimu ya kifedha na ushauri wa kitaalamu utakaowasaidia wanufaika kusimamia vizuri biashara zao na kurejesha mikopo kwa wakati.
Baadhi ya vijana walionufaika na awamu ya kwanza ya mikopo hiyo walieleza kufurahishwa na kuanza kwa programu hiyo, wakisema imewapa matumaini mapya ya kutimiza ndoto zao za ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi.

Walisema changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ilikuwa ni ukosefu wa mtaji wa kuanzisha au kupanua biashara, hivyo mikopo hiyo imekuja wakati muafaka. Walieleza kuwa wataitumia kwa uwajibikaji na kwa shughuli zilizokusudiwa ili kuongeza uzalishaji, kukuza biashara zao na kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana wengine.
Aidha, waliishukuru Serikali kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Benki ya CRDB kwa kushiriki katika utekelezaji wa programu hiyo, wakiahidi kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha vijana wengine kunufaika na fursa hiyo.
Programu ya Shilingi bilioni 200 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana inatarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji, kuimarisha biashara zinazomilikiwa na vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ujasiriamali na ubunifu.
Mwisho….
