MWISHO WA ADHA YA MAJI KIMINDOROSI, WANAWAKE WAMSHUKURU RAIS SAMIA MWENGE WA UHURU WAPITISHA

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha

Wanawake Kimindorosi Wampongeza Rais Samia kwa Kuondoa Kero ya Maji Arusha
Arusha, Julai 9, 2026 – Tabasamu limerejea kwa wanawake wa eneo la Kimindorosi, Mtaa wa Mlimani, Kata ya Olasit katika Jiji la Arusha, baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kukamilisha mradi wa tenki la maji uliomaliza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Wanawake hao wamesema mradi huo umebadili maisha yao kwa kuwa umepunguza muda waliokuwa wakitumia kutafuta maji na kuwawezesha kujikita zaidi katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya familia.

Habari Picha 19217
Habari Picha 19216

Shukrani hizo zimetolewa leo Julai 9, 2026 wakati Mwenge wa Uhuru ulipoweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika eneo la Kimindorosi. Mradi huo unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha huduma za maji kwa wananchi.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, miaka mingi walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji uliowalazimu kutembea umbali mrefu au kununua maji kwa gharama kubwa kutoka kwa wauzaji binafsi. Hali hiyo iliathiri shughuli za kiuchumi na ustawi wa familia nyingi.
Mkazi wa Mtaa wa Mlimani, Mama Jackson, amesema mradi huo umeleta nafuu kubwa kwa wanawake ambao kwa muda mrefu walibeba mzigo mkubwa wa kutafuta maji.

Habari Picha 19218
Habari Picha 19219

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusikiliza. Zamani tulikuwa tunatumia zaidi ya shilingi elfu 60 kwa mwezi kununua maji kutoka kwa wauzaji, huku tukipoteza muda mwingi kuyatafuta. Leo maji yanapatikana nyumbani saa 24, jambo ambalo limerahisisha maisha yetu na kutupa muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.

Naye Elizabeth Emmanuel amesema kuwa kabla ya mradi huo kukamilika, wanawake walilazimika kuvuka Barabara ya East Africa na kupanda maeneo ya mlimani wakiwa wamebeba ndoo za maji kichwani, hali iliyokuwa ikiwachosha na kuhatarisha usalama wao.

Amesema kwa sasa maji yanapatikana moja kwa moja kwenye makazi yao, jambo ambalo limewaondolea adha hiyo na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Kimindorosi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Marita Gido, ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya huduma za msingi inayogusa maisha ya wananchi.

Amesema wanawake ndio walezi wakuu wa familia, hivyo upatikanaji wa maji karibu na makazi yao unawaondolea mzigo wa kutafuta huduma hiyo muhimu na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Habari Picha 19220
Habari Picha 19221

Mradi wa tenki hilo ni sehemu ya miradi inayotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Jiji la Arusha. Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge mwaka 2026,

Mwenge unakimbizwa umbali wa kilomita 89.2 ndani ya jiji hilo na unatembelea jumla ya miradi saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.9.

Utekelezaji wa miradi ya maji unaendelea kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita, ukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao, huku ukiimarisha afya, ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi wa wananchi.

Mwisho…..

Share This Article
Leave a Comment