Na Richard Mrusha
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano , Dkt. Evaline Munisi, leo julai 5, 2026 ametembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu Pamoja na taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi na kutoa maelekezo ya kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Munisi amesema kuwa ameridhishwa na namna wananchi wanavyopata elimu kuhusu haki na wajibu wao katika maeneo ya kazi, ikiwemo masuala ya usalama na afya kazini, pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria za kazi kwa waajiri na wafanyakazi.
Amesema banda hilo limekuwa fursa muhimu ya kusikiliza na kutatua changamoto pamoja na kupokea maoni na malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya Kazi na Ajira, huku wataalamu wakitoa ushauri na ufafanuzi wa sheria na taratibu mbalimbali za Serikali.
Aidha, Dkt. Munisi ameeleza kufurahishwa na elimu inayotolewa kwa vijana, hususan wanawake, kuhusu fursa za kuongeza ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa linaloendeshwa na maendeleo ya teknolojia na ubunifu.
“Leo dunia inahitaji watu wenye ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia. Serikali tayari imeanza kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya stadi na ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa kwa ushindani,” amesema Dkt. Munisi.
Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni ametembelea baadhi ya vituo vya mafunzo ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa programu hizo na kubaini kuwa hatua zinazochukuliwa zinaendelea kuleta matokeo chanya.
Aidha amewahakikishia Watanzania kuwa, kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika maendeleo ya ujuzi na teknolojia, katika miaka michache ijayo nchi itakuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali.
Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi zinazotoa huduma na elimu kwa wananchi.
Mwisho…

