WAFANYA BIASHARA WANAWAKE ZAIDI YA 200 WANUFAIKA NA KIBUBUAPP NDANI NA NJE YA NCHI

a24tv
2 Min Read

Naibu Waziri wa maendeleo ya jamii jinsia Wanawake na makundi Maalumu Mhandisi Marrypriscar Mahundi amesema Serikali Yaendelea Kuwawezesha Wanawake Kupitia Teknolojia na Masoko ya Kidijitali

amesema serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali kupitia upatikanaji wa mitaji, mafunzo na masoko ya bidhaa na huduma zao.

Akijibu swali bungeni, Mahundi amesema kuwa maendeleo ya teknolojia duniani yamefungua fursa mpya kwa wanawake kufanya biashara na kufikia masoko makubwa zaidi ndani na nje ya nchi. Ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wadau mbalimbali kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ( PPP), imeendelea kuhamasisha matumizi ya majukwaa ya kidijitali yanayowawezesha wanawake kufanya biashara kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kuna mifumo na programu mbalimbali zinazowasaidia wanawake kupata masoko na wateja kwa njia ya mtandao. Miongoni mwa mifumo hiyo ni KibubuApp, jukwaa linalowaunganisha wafanyabiashara wadogo na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali.

Amesema kuwa kupitia jukwaa hilo, wanawake wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za kukodi maduka wanaweza kuuza bidhaa zao mtandaoni na kupata wateja kutoka maeneo mbalimbali nchini na hata nje ya mipaka ya Tanzania. Bidhaa zinazouzwa kupitia mfumo huo ni pamoja na viungo, dagaa, bidhaa za kilimo zilizoongezwa thamani na bidhaa nyingine mbalimbali.

“Teknolojia imeondoa vikwazo vingi vya biashara. Mwanamke anaweza kuuza bidhaa zake akiwa nyumbani na kupata masoko mapana zaidi kupitia mifumo ya KibubuApp” amesema Mahundi.

Aidha, Mahundi ameongez kuwa serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya mfumo wa e-Soko, unaowezesha wafanyabiashara na wazalishaji kupata taarifa za bei za bidhaa, mwenendo wa masoko na fursa za biashara kwa wakati.

Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika biashara yana mchango mkubwa katika kuongeza kipato cha wanawake, kukuza ajira na kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Hatua hizo zinaendelea kuonyesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha wanawake wanatumia kikamilifu fursa zinazotokana na mapinduzi ya kidijitali ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Chanzo: Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment