Arusha.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mpango wake wa bima ya lazima kwa wasafiri.
Wameuelezea kuwa imekuwa nyenzo muhimu ya kulinda wageni huku ikichangia kuongeza mapato kwa ajili na kuimarisha sekta ya afya visiwani humo.

Mpango huo wa bima, ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili.
Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato katika sekta ya utalii, ukiingiza takribani dola za Marekani milioni moja (zaidi ya Sh bilioni 2.6) kila mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu manufaa ya mpango huo.
“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC wakilipia dola 22 pekee ili kuhamasisha ushirikiano wa kikanda na kurahisisha usafiri ndani ya jumuiya hiyo.
Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku watoto walio chini ya umri huo wakisamehewa.
Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar.
Amesema jambo hili linapunguza changamoto na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapohitaji.
“Mpango huu unawalinda watalii na wawekezaji dhidi ya gharama zisizotarajiwa za matibabu na changamoto za kiutawala zinazoweza kujitokeza wakati wa safari.
” Unahakikisha wageni wanapata msaada wa haraka kupitia vituo maalumu vya huduma na taasisi za afya zilizotengwa,” alisema.
Aliongeza kuwa sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia bima hiyo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha sekta ya afya kwa ujumla.
Muhammad alisema mpango huo ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini matukio ya mara kwa mara ambapo watalii na wawekezaji walihitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo.
“Mfuko huu wa bima sasa unasaidia mtandao wa hospitali na vituo vya afya vilivyotengwa kwa ajili ya wageni kote Zanzibar, jambo linalochangia kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha wageni wanapata matibabu bora wanapoyahitaji,” alisema.
Alisema mwitikio wa wananchi na wadau wa utalii kuhusu mpango huo umekuwa chanya, hususan kwa washiriki wa maonesho hayo.
“Tumepokea mrejesho mzuri kutoka kwa wageni na wadau wa utalii wanaotambua umuhimu wa kuwa na mfumo wa uhakika wa kuwahudumia wasafiri,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 inaendelea kuwa maonesho makubwa zaidi ya utalii na biashara Afrika Mashariki, yakileta pamoja wadau wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Alisema maonesho hayo yamevutia waoneshaji, wanunuzi wa huduma za utalii na wataalamu wa sekta hiyo kutoka zaidi ya nchi 40, na hivyo kufungua fursa za uwekezaji, ushirikiano wa kimkakati na upanuzi wa masoko.
“Maonesho haya yanatoa jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa za utalii, kujenga mahusiano ya kibiashara na kuitangaza Tanzania pamoja na Afrika Mashariki katika soko la dunia,” alisema Shoo.
Aliongeza kuwa tukio hilo limewakutanisha zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii 20,000 kutoka mataifa mbalimbali.
“Hali hii inazidi kuimarisha hadhi ya Afrika Mashariki kama kitovu kinachokua kwa kasi katika sekta ya utalii na uwekezaji”.
Mwisho.
