Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kurejesha huduma ya kubadilisha fedha chakavu moja kwa moja kwa wananchi, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki na taratibu za kubadilisha fedha zilizoharibika.

Akizungumza katika Maonesho ya Karibu-KiliFair jijini Arusha, Meneja wa Uendeshaji wa Benki Kuu Tanzania Tawi la Arusha, Critus Joseph Mwakalinga, alisema wananchi sasa wanaweza kufika moja kwa moja katika matawi ya Benki Kuu kwa ajili ya kubadilisha noti zilizochakaa, kuungua au kuchanika, mradi zitimize vigezo vilivyowekwa.
Alisema hapo awali huduma hiyo ilitolewa zaidi kupitia benki za biashara, lakini sasa Benki Kuu imeongeza wigo wa huduma hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Vigezo vya Kubadilisha Fedha Chakavu
Mwakalinga alisema noti inayowasilishwa kwa ajili ya kubadilishwa lazima kwanza iwe noti halali ya Tanzania. Noti bandia haiwezi kubadilishwa kwa sababu haina thamani inayotambulika kisheria.
Aidha, noti hiyo inapaswa kuwa imebakiza angalau asilimia 75 ya eneo lake la awali. Ikiwa noti imechanika vipande viwili, vipande hivyo lazima viwe vya noti moja na ya thamani moja.
Benki Kuu pia hukagua uwepo wa alama muhimu za noti ikiwemo maandishi ya “Benki Kuu ya Tanzania”, thamani ya noti, namba za utambulisho pamoja na sahihi za Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Fedha.
Wananchi wanaotaka kubadilisha noti hizo wanatakiwa kuwasilisha kitambulisho kinachotambulika kisheria kama NIDA, leseni ya udereva au barua ya utambulisho wa mkazi pamoja na kujaza fomu maalum ya maombi.

Utaratibu wa Fedha Zilizoungua
Kwa fedha zilizoharibika kutokana na majanga ya moto, mwombaji atalazimika kuwasilisha uthibitisho kutoka kwa mtendaji wa eneo husika pamoja na taarifa kutoka Jeshi la Polisi kuthibitisha tukio hilo kabla ya fedha hizo kufanyiwa tathmini.
Benki Kuu imesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma hiyo haitumiki vibaya na kuzuia vitendo vya udanganyifu au utakatishaji fedha.
Onyo kwa Wanaoharibu Fedha kwa Makusudi
Wakati huo huo, Benki Kuu imetoa onyo kali kwa wananchi wanaoharibu noti kwa makusudi, ikisisitiza kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai linaloweza kusababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mhusika.
Mwakalinga alisema noti ambazo zitabainika kukatwa, kuchanwa au kuharibiwa kwa makusudi hazitastahili kubadilishwa. Aidha, mtu atakayebainika kuwasilisha noti bandia hataweza kupata fidia yoyote kutoka Benki Kuu.
“Kuharibu fedha za Tanzania kwa makusudi ni kosa la jinai. Tunawaomba wananchi kuzitunza fedha zao na kufuata taratibu rasmi wanapohitaji kubadilisha fedha zilizoharibika,” alisema.
Aliongeza kuwa huduma hiyo inalenga kuwasaidia wananchi waliopata hasara kutokana na ajali au majanga yasiyokuwa ya makusudi, na si wale wanaoharibu fedha kwa makusudi.
Benki Kuu imewahimiza wananchi kutumia matawi yake pamoja na benki za biashara zilizoidhinishwa kupata huduma za kubadilisha fedha chakavu na kuendelea kutafuta elimu ya fedha ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kusababisha upotevu wa fedha.

