POLISI ARUSHA YAIMARISHA OPERESHENI YA USALAMA BARABARANI KUELEKEA MWISHO WA MWAKA.

Geofrey Steven
2 Min Read

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha limeimarisha operesheni maalumu ya ukaguzi wa vyombo vya moto na madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia ajali katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka na likizo za wanafunzi.

Akizungumza wakati wa operesheni hiyo inayoendelea mkoani humo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, ACP Zauda Mohamed, amesema hatua hiyo imekuja kutokana na ongezeko la abiria na vyombo vya moto barabarani katika kipindi hiki, hali inayohitaji kuimarishwa kwa uangalizi na ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.

Habari Picha 22309

Amesema katika operesheni hiyo, jeshi hilo limejikita katika kubaini makosa mbalimbali ya barabarani, yakiwemo mwendo kasi, uendeshaji wa magari ukiwa umelewa, ubovu wa vyombo vya moto pamoja na ukaguzi wa mabasi ya masafa marefu ili kuhakikisha yanazingatia matakwa ya kuwa na madereva wawili kwa safari ndefu.

ACP Zauda ameeleza kuwa madereva waliobainika kutokidhi vigezo vya usalama wamechukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, huku wengine wakipewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Habari Picha 22310

Amesisitiza kuwa madereva wanapaswa kuwa makini, kuepuka vitendo hatarishi na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.

Katika hatua nyingine, ACP Zauda amewataka wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto wao katika kipindi cha likizo kinachotarajiwa kudumu takribani miezi miwili, akiwataka kuhakikisha watoto wanapata uangalizi wa kutosha wanapotumia barabara, iwe kwa kutembea kwa miguu au kusafiri kama abiria.

Habari Picha 22311

Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kutunza funguo za magari na pikipiki zao katika sehemu salama zisizoweza kufikiwa na watoto, akieleza kuwa kumekuwa na taarifa za ajali zinazohusisha wanafunzi wanaochukua funguo za vyombo hivyo bila ruhusa na kuviendesha barabarani.

Amesisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja, hivyo madereva, wazazi, walezi na watumiaji wengine wa barabara wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na likizo kinapita kwa amani bila ajali zinazoweza kuepukika.

Habari Picha 22312

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment