Na Geofrey Stephen Arusha .
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewahimiza vijana nchini kujitokeza na kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya kilimo cha bustani (Horticulture), akieleza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za ajira, kujiajiri na kukuza biashara.
Chongolo amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na biashara ya mazao ya bustani katika soko la kimataifa kupitia jukwaa la HortiLogistica Africa 2026, linalolenga kuwaunganisha wakulima, wafanyabiashara, wawekezaji na wanunuzi wa mazao kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Amesema vijana hawapaswi kuangalia kilimo cha bustani kama shughuli ya kulima na kuvuna pekee, bali wanapaswa kuona fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani, ikiwamo uzalishaji wa miche bora, uvunaji, uchakataji, ufungashaji na usafirishaji wa mazao.
HORTILOGISTICA FURSA YA KUITANGAZA TANZANIA DUNIANI
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya washiriki wa maonesho hayo katika viwanja vya TGT, eneo la Bulka jijini Arusha, Chongolo alisema jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika soko la dunia.

Alisema maonesho hayo yatasaidia kuwaunganisha wazalishaji wa ndani na wanunuzi wa kimataifa, kubadilishana uzoefu na kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania inahitaji kuondoka katika mfumo wa kuzalisha na kuuza mazao ghafi na kuelekea kwenye kilimo cha kisasa kinachozingatia teknolojia, ubora, uchakataji na mahitaji ya masoko ya kimataifa.
Alisisitiza pia umuhimu wa wakulima kuzingatia viwango vya kimataifa, kuongeza tija na kuboresha mifumo ya usafirishaji ili mazao ya Tanzania yaweze kushindana katika masoko ya nje.
VIJANA WANAWEZA KUTENGENEZA AJIRA KUPITIA KILIMO CHA BUSTANI
Kilimo cha bustani kimeendelea kuwa eneo lenye fursa mbalimbali za kiuchumi, hususan kwa vijana wanaotafuta njia za kujiajiri na kuanzisha biashara.
Kupitia maonesho hayo, vijana wanapata nafasi ya kujifunza namna wanavyoweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kilimo cha bustani, bila kutegemea kumiliki mashamba makubwa.
Fursa hizo zinajumuisha biashara ya miche, huduma za pembejeo, teknolojia za kilimo, uchakataji wa matunda na mboga, ufungashaji pamoja na biashara ya kusafirisha mazao katika masoko ya kimataifa.
AFRICADO: PARACHICHI NI FURSA YA DHAHABU KWA VIJANA
Miongoni mwa kampuni zilizoshiriki maonesho hayo ni Africado Company Limited ya Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, inayojihusisha na kilimo cha parachichi na kuhudumia zaidi ya wakulima wadogo 2,000 katika Kanda ya Kaskazini.
Meneja wa kampuni hiyo, Vincent Marisha, amesema kilimo cha parachichi ni fursa adhimu kwa vijana kutokana na uwezekano wa kupata kipato kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na zao hilo.
“Kwa upande wa parachichi, naweza kusema ni fursa adhimu au dhahabu kwa vijana. Wengi sasa wana mwamko wa kulima, na ningependa kuwashauri kuwa kilimo cha parachichi kinalipa,” alisema Marisha.
Amesema Africado imekuwa ikiwasaidia wakulima wadogo kwa kuwapatia miche, elimu ya kanuni bora za kilimo na kuwaunganisha na masoko, huku kampuni hiyo ikisafirisha parachichi katika masoko ya Ulaya, Asia na India.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kutazama fursa za parachichi kwa upana zaidi, badala ya kujikita katika uzalishaji pekee, kwani uchakataji na biashara ya zao hilo pia vina nafasi kubwa ya kuingiza kipato.
NCHI TAKRIBANI 40 KUSHIRIKI HORTILOGISTICA AFRICA 2026
HortiLogistica Africa 2026 linatarajiwa kushirikisha washiriki kutoka takribani nchi 40 na zaidi ya wageni 3,000, likiwa na lengo la kuifanya Arusha kuwa jukwaa muhimu la biashara, teknolojia na uwekezaji katika sekta ya kilimo cha bustani barani Afrika.
Maonesho hayo yanahusisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji wa miche, kilimo, uvunaji, uchakataji, ufungashaji hadi usafirishaji wa mazao kwenda katika masoko ya nje.
Tanzania inaendelea kutafuta nafasi kubwa zaidi katika biashara ya kimataifa ya mazao ya bustani, yakiwamo parachichi, maua, mboga na matunda, ambayo yana uwezo wa kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi.
Ujumbe mkuu kwa vijana ni kwamba kilimo cha bustani si kulima pekee; ni biashara yenye fursa nyingi kuanzia shambani hadi katika soko la kimataifa.
Mwisho.
