Na Geofrey A24tv.
ARUSHA:
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amewakaribisha wawekezaji, wafanyabiashara, wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka ndani na nje ya nchi kushiriki Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, litakalofanyika kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2026, katika viwanja vya TGT jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumamosi Novemba 7, 2026, katika viwanja vya TGT, CPA Makalla amesema jukwaa hilo litafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ambaye atakuwa mgeni rasmi.

Amesema ushiriki wa Makamu wa Rais katika ufunguzi wa jukwaa hilo unaonesha umuhimu wa sekta ya kilimo cha bustani (Horticulture) katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira, kupanua wigo wa biashara na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa HortiLogistica Africa 2026 ni fursa muhimu ya kiuchumi kwa Arusha, ikitarajiwa kuwakutanisha waoneshaji zaidi ya 150 kutoka Afrika, Ulaya na Asia, pamoja na wageni zaidi ya 3,000 kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.


Amebainisha kuwa jukwaa hilo halitakuwa fursa kwa wadau wa kilimo pekee, bali pia litachochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo hoteli, usafirishaji, utalii, biashara na huduma mbalimbali, kutokana na ongezeko la wageni na wawekezaji watakaotembelea mkoa huo.
Aidha, CPA Makalla amesema kupitia jukwaa hilo, Arusha itaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara, uwekezaji na mikutano ya kimataifa, huku akiwahakikishia washiriki wote usalama na mazingira rafiki wakati wote wa shughuli za jukwaa hilo.
Amewataka wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali wa Arusha kutumia kikamilifu fursa zitakazojitokeza, ikiwemo kutangaza bidhaa na huduma zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kuanzisha mahusiano yatakayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi hata baada ya kumalizika kwa jukwaa hilo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kilimo cha Bustani Tanzania (TAHA), Dkt. Jackline Mkindi, amesema lengo kuu la HortiLogistica Africa 2026 ni kuwaunganisha wakulima wa Tanzania na masoko ya kimataifa, teknolojia za kisasa, wawekezaji pamoja na watoa huduma za usafirishaji wa mazao.

Amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa wakulima na wadau wengine kujifunza mbinu mpya za uzalishaji, kuongeza ubora na thamani ya mazao, pamoja na kupata fursa za kibiashara zitakazowawezesha kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Dkt. Mkindi amesisitiza kuwa kuimarisha uhusiano kati ya wakulima, wawekezaji na masoko ni hatua muhimu katika kukuza sekta ya kilimo cha bustani na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania.

HORTILOGISTICA AFRICA 2026: FURSA YA KIMATAIFA, UWEKEZAJI NA MASOKO KWA WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa daraja muhimu la kuunganisha wazalishaji wa mazao ya bustani na fursa za biashara za kimataifa, huku likiipa Arusha nafasi ya kunufaika na uwekezaji, utalii na shughuli mbalimbali za kiuchumi.



#HortiLogisticaAfrica2026 #Arusha #TAHA #KilimoBiashara #Uwekezaji #Tanzania
