DCEA YAGEUKIA MFUMO WA MATIBABU BADALA YA ADHABU KWA WARAIBU WANAOKINZANA NA SHERIA..

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Mwandishi wa A24tv.

ARUSHA:

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, wataalamu wa afya pamoja na mashirika ya kijamii wameungana kuimarisha mfumo wa Deflection, unaolenga kuwasaidia watu wenye uraibu wa dawa za kulevya wanaokinzana na sheria kupata matibabu na huduma za kisaikolojia badala ya kutegemea adhabu pekee.

Akizungumza jijini Arusha, Kamishna wa DCEA, Hussein Mbaga, aliyemwakilisha Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, amesema uraibu wa dawa za kulevya ni changamoto ya kiafya inayohitaji kushughulikiwa kwa njia ya matibabu, ushauri nasaha na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Habari Picha 22251

Amesema mfumo huo wa Deflection una nafasi kubwa katika kupunguza uhalifu mdogo unaohusiana na matumizi ya dawa za kulevya, kupunguza msongamano katika mahakama na magereza, pamoja na kuokoa maisha ya watu wanaokabiliwa na changamoto ya uraibu.

Kwa upande wake, Kiongozi wa PTACC Afrika, Dkt. Yvonne Olando, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya sheria, wataalamu wa afya na jamii katika kuhakikisha watu wenye uraibu wanapata msaada unaostahili.

Habari Picha 22252
Habari Picha 22253

Ameeleza kuwa ni muhimu kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wenye uraibu wa dawa za kulevya na kuhakikisha mfumo wa Deflection unatambulika, unaimarishwa na kutekelezwa kwa viwango vinavyofanana katika mataifa mbalimbali barani Afrika.

Naye Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Henry Mwaibambe, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutambua umuhimu wa kuwabaini mapema watu wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwaunganisha na huduma za matibabu na usaidizi wa kitaalamu.

Amebainisha kuwa kupitia mfumo wa Polisi Kata unaofikia kata 3,956 Tanzania Bara na shehia 358 Zanzibar, kuna fursa kubwa ya kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na jamii katika kuwafikia watu wanaohitaji msaada.

Habari Picha 22254
Habari Picha 22255

Aidha, amezitaka familia kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa na kutafuta msaada mapema pale zinapobaini ndugu zao wanakabiliwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, ili hatua stahiki zichukuliwe kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Kongamano hilo la siku mbili la PTACC Africa Deflection Summit, linalofanyika Novemba 5 hadi 6, 2026, katika Ukumbi wa Corridor Spring Hotel jijini Arusha, limewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka katika vyombo vya sheria, taasisi za afya na mashirika ya kiraia.

Washiriki hao wanajadili mikakati ya kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya, kukabiliana na vifo vinavyotokana na matumizi ya dawa kupita kiasi (overdose), pamoja na kuimarisha mifumo ya kuwaunganisha watu wenye uraibu na huduma za matibabu na msaada wa kisaikolojia.

Habari Picha 22256
Habari Picha 22257
Habari Picha 22258

Kupitia kongamano hilo, wadau wameendelea kusisitiza kuwa mtu mwenye uraibu wa dawa za kulevya anahitaji nafasi ya kupata matibabu, kurekebisha maisha yake na kurejea katika jamii. Hivyo, ushirikiano wa familia, jamii, vyombo vya sheria na wataalamu wa afya ni muhimu katika kupambana na changamoto hiyo.

Habari Picha 22259
Habari Picha 22260
Habari Picha 22261

UJUMBE MKUU: Uraibu wa dawa za kulevya unahitaji kushughulikiwa kwa mtazamo wa afya na utu. Kutoa msaada, matibabu na fursa ya kurejea katika jamii ni sehemu muhimu ya kujenga jamii salama na yenye matumaini.

KataaDawaZaKulevya #TimizaMalengoYako #DCEA #

Share This Article
Leave a Comment