Na Geofrey Stephen
Hai, Kilimanjaro
Mradi wa EASTRIP unaotekelezwa katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Kampasi ya Kikuletwa, unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, 2026, huku ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa maji wenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.65 ukifikia hatua za mwisho. Mtambo huo unatarajiwa kuimarisha mafunzo ya vitendo na kuongeza uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya nishati nchini.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi ili kuandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo iliyoshirikisha wawakilishi wa Serikali, Benki ya Dunia na viongozi wa taasisi zinazotekeleza mradi,
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa EASTRIP, Dkt. Frederick Salukele, amesema awamu ya kwanza ya mradi imefikia asilimia 99 ya ukamilishaji.
Amesema awamu hiyo inahusisha ufungaji wa mashine za kufua umeme na mifumo ya kupokea maji, huku awamu ya pili ikihusisha ujenzi wa miundombinu ya kiraia na mifumo ya kuingiza maji kwenye mtambo ili kuwezesha uzalishaji wa umeme.
Dkt. Salukele ameeleza kuwa baada ya mifumo hiyo kukamilishwa na kuunganishwa, umeme utakaotokana na mtambo huo utaweza kuunganishwa kwenye gridi ya taifa kupitia miundombinu ya kilovolti 33.

Amesema mradi huo upo katika mwaka wake wa mwisho na unatarajiwa kufungwa rasmi Desemba 31, 2026, akisisitiza kuwa kufungwa kwa mradi hakutamaanisha kusimama kwa shughuli za mafunzo, bali kutakuwa mwanzo wa matumizi endelevu ya miundombinu hiyo katika kutoa mafunzo ya vitendo kwa vijana.
Ameongeza kuwa mtambo huo utawasaidia wanafunzi kujifunza namna ya kuendesha na kusimamia mitambo ya kuzalisha umeme, pamoja na kuelewa taratibu za kuunganisha umeme kwenye gridi ya taifa.


Kwa mujibu wa Dkt. Salukele, uwekezaji huo unaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususan katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na kuongeza mchango wa shughuli za uzalishaji katika uchumi wa taifa.
Aidha, amewahimiza vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ili kupata maarifa na ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya nchi.
ATC YAWEKA MKAZO KATIKA MAFUNZO YA NISHATI SAFI.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Musa Chacha, amesema mtambo huo utakuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha mafunzo ya vitendo, kuandaa wataalamu wa sekta ya nishati na kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Chacha ameeleza kuwa ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa uchumi vinaongeza mahitaji ya nishati ya uhakika, hivyo taasisi za elimu ya ufundi zina wajibu wa kuandaa vijana wenye uwezo wa kuzalisha na kusimamia mifumo mbalimbali ya nishati.
Amesema chuo kina jukumu la kutoa mafunzo katika teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa umeme, zikiwemo nishati ya maji, jua, upepo na teknolojia zinazotumia taka.



Ameongeza kuwa kupitia mtambo huo, wanafunzi hawataishia kujifunza nadharia pekee, bali watapata nafasi ya kufanya mazoezi katika mazingira halisi ya uzalishaji wa umeme, kujifunza uendeshaji wa mashine na mifumo yake, pamoja na kuzingatia taratibu za usalama na usimamizi wa mitambo.
Kwa mujibu wa uongozi wa chuo, uwekezaji huo utaongeza uwezo wa ATC kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuvutia wanafunzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Uongozi huo umeishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu hiyo, huku ukisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mtambo unakamilika na kuendelea kutumika kwa mafunzo hata baada ya mradi kufungwa rasmi.
BENKI YA DUNIA YAPONGEZA MABORESHO YA ELIMU YA UFUNDI.
Naye Mtaalamu wa Ujuzi kutoka Benki ya Dunia, Nkahiga Kaboko, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua zilizopigwa katika kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi kupitia maboresho ya mitaala, vifaa vya kufundishia na mafunzo ya walimu katika ngazi mbalimbali za elimu.
Kaboko amesema uwekezaji huo umeimarisha uwezo wa taasisi za mafunzo kutoa elimu inayozingatia mahitaji ya soko la ajira, akieleza kuwa changamoto ya ajira kwa vijana inapaswa kuangaliwa pia kwa kuzingatia ubora wa ujuzi walionao wahitimu.



Amesema baadhi ya vijana hukabiliwa na changamoto ya kutokuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya waajiri, hivyo uwekezaji katika mafunzo ya vitendo na teknolojia za kisasa ni muhimu katika kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Amewahimiza waajiri kushirikiana na taasisi za elimu ya ufundi kwa kutoa maoni kuhusu ujuzi unaohitajika, kutumia fursa zinazotolewa na miundombinu hiyo na kusaidia kuwaandaa vijana kwa mazingira halisi ya kazi yanayokidhi viwango vya kikanda na kimataifa.
Akitoa mfano wa sekta ya usafiri wa anga,
Kaboko amesema wahitimu wa mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Usafirishaji ya Taifa (NIT) wamepata fursa za kufanya kazi ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa elimu ya ufundi yenye ubora inaweza kufungua milango ya ajira katika soko la kimataifa.


Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha miundombinu na vifaa vilivyowekwa kupitia EASTRIP vinaendelea kufanya kazi baada ya mradi kukamilika, ikiwemo maandalizi ya rasilimali za uendeshaji na matengenezo.
WATAALAMU WA KITANZANIA WASIMAMIA UJENZI WA MTAMBO.
Katika hatua nyingine, mtaalamu anayesimamia kitengo cha umeme katika mradi huo, Aizack Legonda, amesema usimamizi wa ujenzi umefanywa na wataalamu wa Kitanzania kutoka Consulting Bureau ya Arusha Technical College, kwa kushirikiana na wataalamu wenye uzoefu kutoka Tanroads Engineering Consulting Unit na walioshiriki katika usimamizi wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Amesema ushirikiano huo umewezesha kuhamisha uzoefu na maarifa yaliyopatikana katika miradi mikubwa ya nishati na kuyatumia katika utekelezaji wa mradi wa EASTRIP.



Kwa mujibu wa Legonda, awamu ya kwanza ya mradi imefikia asilimia 99 ya ukamilishaji, huku awamu ya pili, inayohusisha ujenzi wa miundombinu ya kiraia ikiwemo bwawa dogo la kuelekeza maji kwenye mtambo, ikiwa imefikia asilimia 45.
Amesema kukamilika kwa kazi zilizobaki kutawezesha mtambo kuanza kuzalisha umeme wa megawati 1.65 na kutoa fursa ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi katika mazingira halisi ya uzalishaji wa umeme wa maji.
Amesisitiza kuwa Tanzania ina wataalamu wenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza miradi ya teknolojia ya umeme wa maji, hivyo ni muhimu kuwapa nafasi ya kutumia ujuzi wao katika miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, amesema hatua za kiusalama zimechukuliwa katika eneo la ujenzi, ikiwemo kuweka kingo na mifumo ya kuelekeza maji ili kuzuia maji kuathiri kazi zinazoendelea na kuhakikisha kazi zilizobaki zinafanyika kwa usalama.
EASTRIP KULENGA UENDELEVU WA MAFUNZO NA AJIRA.
Mradi wa EASTRIP unatekelezwa katika nchi tatu, ikiwemo Tanzania, kwa lengo la kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi na kuongeza uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta muhimu za uchumi.
Nchini Tanzania, taasisi zinazotekeleza mradi huo ni Arusha Technical College (ATC), Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) na National Institute of Transport (NIT).
Kupitia uwekezaji huo, taasisi hizo zinalenga kuimarisha ubora wa mafunzo, kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja katika soko la ajira.



Kukamilika kwa mtambo wa kufua umeme katika Kampasi ya Kikuletwa ya ATC kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuunganisha elimu ya nadharia na mafunzo ya vitendo, huku uendelevu wa matumizi yake ukiwa muhimu katika kuhakikisha manufaa ya mradi yanaendelea kuonekana hata baada ya kufungwa rasmi.
Mafanikio ya muda mrefu ya uwekezaji huo yatategemea kukamilika kwa kazi zilizobaki, upatikanaji wa rasilimali za uendeshaji na matengenezo, pamoja na matumizi endelevu ya mtambo huo katika mafunzo na ukuzaji wa ujuzi wa wataalamu wa sekta ya nishati nchini.


Mwisho…
