Na Geofrey Stephen ARUSHA:
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara za Kona ya Nairobi–Kisongo na Kona ya Nairobi–Soko la Kilombero anasimamiwa kwa karibu ili miradi hiyo ikamilike ifikapo Desemba mwaka huu.
Naibu Waziri Kasekenya ametoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo jijini Arusha, zinazotekelezwa na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG).


Amesema kukamilika kwa barabara hizo kwa wakati na kwa ubora ni muhimu katika maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON, huku akisisitiza kuwa miundombinu hiyo itaendelea kuwa na manufaa kwa wananchi hata baada ya mashindano kumalizika.
“AFCON ni fursa muhimu kwa taifa. Hivyo, barabara hizi zikikamilika kwa ubora, licha ya kurahisisha usafiri wakati wa michuano hii, pia zitaongeza mtandao wa barabara jijini Arusha na kuchochea fursa za kiuchumi,” amesema Eng. Kasekenya.



Amesema maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha miradi hiyo haikwami na inakamilika ndani ya muda uliopangwa.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba hii miradi isikwame, ikamilike ndani ya muda na kwa upande wetu, ndani ya muda ni Desemba mwaka huu,” amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Barabara zitaongeza hadhi ya Arusha.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, ujenzi wa barabara hizo hauishii katika uwekaji wa lami pekee, bali unajumuisha pia njia za watembea kwa miguu pamoja na taa za barabarani, hatua inayolenga kuboresha mandhari na usalama wa jiji la Arusha.
“AFCON ni ya muda mfupi, lakini miundombinu itaendelea kubaki na kwa muda mrefu,” ameongeza Eng. Kasekenya.
Aidha, amezitaka taasisi zinazohusika na huduma za maji, umeme na mawasiliano kushirikiana kwa karibu na wakandarasi ili kuhakikisha miundombinu ya chini ya ardhi, ikiwemo mabomba na nyaya, inahamishwa kwa haraka katika maeneo yenye ujenzi.
Amesema ushirikiano huo utasaidia kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi na kuwezesha mkandarasi kwenda sambamba na kasi iliyowekwa na Serikali.
Ujenzi kuendelea usiku
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Reginald Masawe, amemhakikishia Naibu Waziri kuwa wataendelea kusimamia ujenzi huo kwa karibu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Amesema kwa sasa ujenzi unaendelea kwa kasi, ikiwa ni pamoja na kazi kufanyika nyakati za usiku, kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na miundombinu hiyo kiuchumi na kijamii.
Sh10.2 bilioni zimetolewa kama fidia



Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa jumla ya Sh10.2 bilioni zimetumika kulipa fidia kwa wananchi 48 waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Kukamilika kwa barabara hizo kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri ndani ya Jiji la Arusha, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi, huku miundombinu hiyo ikiwa sehemu ya maandalizi ya jiji kwa shughuli zinazohusiana na AFCON.



Mwisho…
