Na Geofrey Stwphen Arusha .
Arusha.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewataka wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini kubadili mtazamo wa kazi zao na kuwa washauri wa kimkakati wanaoweza kuleta mageuzi ya uchumi kupitia usimamizi bora wa fedha za umma.
Ujumbe huo ulitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania hayatategemei ukubwa wa bajeti pekee bali namna inavyosimamiwa.

Alisema uzoefu alioupata katika ziara zake nchini Estonia, Finland na Albania umeonyesha kuwa nchi zinaweza kufikia maendeleo makubwa hata zikiwa na rasilimali chache, mradi watumishi wa umma wafanye maamuzi sahihi na kusimamia matumizi ya fedha kwa uadilifu.
“Ni uchaguzi wa kila mmoja kufanya jambo sahihi au kutolifanya. Wataalamu wa ununuzi waliopo hapa ndiyo wanaoweza kubadili maisha ya Watanzania kupitia maamuzi wanayofanya kila siku,” alisema.
Bajeti kubwa inahitaji uwajibikaji mkubwa
Akieleza mabadiliko ya uchumi wa Tanzania, alisema bajeti ya Serikali imeongezeka kutoka takribani Shilingi bilioni 600 mwaka 1995 hadi zaidi ya Shilingi trilioni 56 katika mwaka wa fedha wa sasa.

Kwa mujibu wake, ongezeko hilo linaonyesha kuwa Serikali imeweka rasilimali za kutosha kwa ajili ya maendeleo, lakini mafanikio yatategemea jinsi fedha hizo zitakavyotumika.
“Fedha hizi ni nyingi. Changamoto siyo ukubwa wa bajeti, bali namna tunavyozitumia kuhakikisha kila shilingi inaleta matokeo yaliyokusudiwa,” alisema
Mtaalamu wa ununuzi asiwe msimamizi wa zabuni pekee.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema wakati umefika kwa wataalamu wa ununuzi kuacha kujiona kama wasimamizi wa taratibu za zabuni pekee na badala yake wawe washauri wa viongozi wa taasisi katika masuala ya masoko, thamani ya fedha, usimamizi wa vihatarishi, ubora wa bidhaa na huduma pamoja na usimamizi wa mikataba.
Alisisitiza kuwa ushauri wa kitaalamu lazima uzingatie sheria, ushahidi na maslahi ya umma ili kuongeza tija katika matumizi ya fedha za Serikali.
Aidha, alisema Serikali tayari imeweka mazingira mazuri kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 3 ya mwaka 2023 pamoja na mfumo wa kielektroniki wa NeST, hivyo jukumu lililobaki ni kwa wataalamu kuhakikisha mifumo hiyo inatumika ipasavyo kuongeza uwazi, ushindani na uwajibikaji.
PPRA yaahidi kuendelea kuimarisha NeST
Alisema PPRA itaendelea kuboresha mfumo wa NeST ili uwe nyenzo muhimu ya kusimamia ununuzi wa umma na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Pia aliwataka wataalamu kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mipango ya ununuzi, matumizi ya mfumo wa NeST, usimamizi wa mikataba, utoaji wa matamko ya mgongano wa maslahi, ushirikishwaji wa makundi maalumu pamoja na kufunga hoja za ukaguzi kwa wakati.
APSP yapitisha maazimio ya kuboresha taaluma.
Katika mkutano huo, wanachama wa APSP walipitisha maazimio kadhaa yatakayolenga kuongeza ufanisi wa ununuzi wa umma nchini.
Maazimio hayo yanajumuisha kuoanisha mipango ya ununuzi na bajeti za taasisi,
kufanya tafiti za soko kabla ya kuanza manunuzi, kutumia njia sahihi za ununuzi na kuhakikisha matangazo ya General Procurement Notices (GPNs) yanaendelea kuchapishwa kupitia mfumo wa NeST hadi hatua zote za zabuni zikamilike.

Viongozi wa chama pia walisisitiza umuhimu wa uwazi katika michakato ya ununuzi kwa kuhakikisha washiriki wote wanatoa matamko ya mgongano wa maslahi, mikataba inasimamiwa ipasavyo na bidhaa pamoja na huduma zinazopokelewa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wa makundi maalumu, APSP ilizitaka taasisi zote kutekeleza matakwa ya sheria ya kutenga asilimia 30 ya fursa za ununuzi kwa makundi hayo na kurekebisha mipango ambayo haikuzingatia sharti hilo.
Mafunzo yaendelee, vikwazo viondolewe
Katika mapendekezo yao kwa PPRA, viongozi wa APSP waliomba ushirikiano zaidi katika utoaji wa mafunzo, tafiti na uandaaji wa miongozo ya ununuzi.
Walipendekeza pia gharama za baadhi ya mafunzo ya kitaaluma zipunguzwe ili wataalamu wengi zaidi waweze kushiriki, pamoja na kuboreshwa kwa nyaraka za zabuni zinazotumika kwa makundi maalumu.
Aidha, walieleza wasiwasi kuhusu baadhi ya waajiri kuwazuia wataalamu kuhudhuria mafunzo ya kitaaluma kwa kisingizio cha ukosefu wa bajeti, wakisema hali hiyo inakwamisha maendeleo ya taaluma wakati sheria na mifumo ya ununuzi inaendelea kubadilika kwa kasi.
Ushirikiano wa PPRA na APSP waimarishwa
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA aliahidi kuendelea kushirikiana na APSP katika kujenga uwezo wa wataalamu, kuboresha miongozo ya ununuzi na kuendeleza matumizi ya mfumo wa NeST.
Alisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kujenga wataalamu wenye uwezo wa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwenyekiti wa APSP Akihitimisha mkutano huo, aliwataka wataalamu wa ununuzi kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya Tanzania.

“Kila uamuzi mnaoufanya unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa taasisi, uchumi wa taifa na maisha ya wananchi. Hilo ndilo jukumu kubwa ambalo mnalibeba,” alisema.
Mwisho .
