Moshi, Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava, ameitaka jamii ya mkoa wa Kilimanjaro kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti, akisisitiza kuwa vitendo hivyo si sehemu ya mila wala utamaduni wa mkoa huo.
Kauli hiyo imetolewa Machi 15, 2026 wakati wa mashindano ya usomaji wa Qur’an kwa watoto na watu wazima yaliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kupitia Idara ya Daawa mkoa wa Kilimanjaro. Mashindano hayo yalifanyika katika ofisi za BAKWATA mkoani humo na kuhudhuriwa na waumini, viongozi wa dini pamoja na viongozi wa serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mzava alisema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia ambayo hapo awali hayakuwa yakishuhudiwa mara kwa mara katika mkoa huo, hivyo jamii inapaswa kusimama pamoja kupambana na vitendo hivyo.
“Kupitia hadhara hii naendelea kusisitiza kuwa mkoa huu haukuwa na tabia ya ubakaji na ulawiti. Hata hivyo, ninapopitia taarifa mbalimbali nakuta matukio hayo sasa yanatokea hata ndani ya familia,” alisema Mzava.
Alieleza kuwa matukio hayo yanaumiza sana jamii kwani wakati mwingine yanahusisha ndugu wa karibu, jambo linalosababisha maumivu makubwa kwa wahanga na familia zao.

“Inasikitisha kuona wakati mwingine mjomba anamlawiti mtoto wa dada yake. Haya hayakuwa mambo yetu katika mkoa huu. Ni muhimu sasa kuilea vizuri jamii yetu, watoto wetu na vijana wetu ili kuepuka matatizo haya,” aliongeza.
Mzava alisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaacha majeraha makubwa kwa wahanga na vinaweza kusababisha chuki katika jamii, hasa pale wahanga wanapotamani kulipiza kisasi kutokana na maumivu waliyopitia.
“Hatutakubali kukaa kimya na kuona mambo haya yanaendelea. Ni lazima tulinde kizazi chetu ili kibaki salama. Tukiona jambo lolote la aina hii, ni muhimu kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ikiwemo Polisi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kilimanjaro, Awazi Lema, aliwaomba wazazi kuwa karibu zaidi na watoto wao na kuwafuatilia kwa karibu, hususan wanaporudi nyumbani wakitoka shuleni.
Alisema ni muhimu wazazi kuwachunguza watoto wao mara kwa mara na kujenga mazoea ya mawasiliano ya karibu ili waweze kugundua mapema dalili zozote za ukatili au vitendo visivyo salama.
Aidha, aliwataka viongozi wa misikiti mkoani humo kuendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo na kuwapa watoto elimu pamoja na mbinu za kujilinda dhidi ya watu wenye nia mbaya.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, aliyekuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo, alisema kuwa elimu ya dini ni muhimu katika kumjenga mtu kutambua mema na mabaya.
Alieleza kuwa mtu asiye na mafunzo ya dini anaweza kukosa mipaka ya maadili na hivyo kujikuta akijihusisha na vitendo viovu kama ubakaji na ulawiti.


Awali, katika risala iliyosomwa na Katibu wa Idara ya Daawa mkoa wa Kilimanjaro, Salmu Muhidini, ilielezwa kuwa idara hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa usafiri wa uhakika ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Akijibu hoja hiyo, mgeni rasmi aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto hiyo, ikiwemo kusaidia kupatikana kwa gari aina ya Noah ili kurahisisha shughuli za idara hiyo.


Mwishoo

