SIHA, Kilimanjaro – Machi 10, 2026.
Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, amewaomba walimu kuzingatia ratiba za masomo zilizowekwa na Serikali ili kuondoa changamoto inayowafanya wanafunzi kuchelewa kufika nyumbani, jambo linalowakosesha fursa ya kusaidia kazi ndogo ndogo za nyumbani pamoja na kuhudhuria madrasa.
Mlewa amesema idadi ya wanafunzi wanaohudhuria madrasa ili kupata elimu ya dini imepungua mkoani Kilimanjaro kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuchelewa kutoka shuleni na kufika nyumbani wakiwa wamechoka.

Amesema baadhi ya shule zimekuwa na utaratibu wa kuwachelewesha wanafunzi kutoka shuleni kwa makusudi, ambapo watoto hutoka saa 11 au hata saa 12 jioni. Hali hiyo husababisha wanafunzi kufika nyumbani wakiwa wamechoka na kukosa muda wa kuwasaidia wazazi au kwenda madrasa kupata elimu ya dini.
Akizungumza Machi 10, 2026, wakati wa mashindano ya usomaji wa Qur’an Tukufu yaliyofanyika katika Msikiti wa Sanya Juu, Wilaya ya Siha, Mlewa alisema ni muhimu walimu kuwapa watoto muda wa kutosha baada ya masomo ili waweze kuhudhuria madrasa na kujifunza dini yao.

“Watoto hawa wanaondoka alfajiri nyumbani na wanaweza kukaa shuleni hadi saa 12 jioni. Anaporudi nyumbani anakuwa amechoka, anatakiwa kuwasaidia wazazi kazi ndogo ndogo za nyumbani na pia kwenda madrasa. Sasa ataweza kuhifadhi Qur’an saa ngapi?” alihoji Mlewa.
Aidha, alisema amepokea taarifa kuwa hata siku za Jumamosi baadhi ya wanafunzi wa darasa la pili, la nne, la saba pamoja na kidato cha pili na cha nne hulazimika kwenda shuleni kwa masomo ya ziada, jambo linalowafanya kukosa kabisa muda wa kupata elimu ya dini.
Aliongeza kuwa hata siku za Jumapili watoto wengi hulazimika kufanya kazi za nyumbani kama kufua nguo, hali inayowafanya washindwe kuhudhuria madrasa.
Kwa mujibu wa Mlewa, hali hiyo inasababisha changamoto katika kuwafundisha watoto maadili na misingi ya dini.
“Tunashindwa kuwahifadhisha Qur’an na kuwafundisha dini yao kwa sababu ya mzigo mkubwa wa masomo wanayopewa. Hata wakati wa likizo bado baadhi yao wanakuwa shuleni,” alisema.
Alitoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuzichunguza shule zinazokiuka utaratibu wa ratiba za masomo na kuhakikisha zinafuata miongozo iliyowekwa ili watoto wapate muda wa kujifunza dini pamoja na kushiriki shughuli za kifamilia.
Katika tukio hilo, Shaabani Muhamedi aliwapongeza waandaaji wa mashindano hayo akisema tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Siha, mashindano kama hayo hayajawahi kufanyika.


Alisema mashindano hayo yalionesha vipaji vya watoto katika usomaji wa Qur’an, ambapo mshindi mmoja mwenye umri wa miaka mitano alifanikiwa kushinda katika kipengele cha usomaji wa Juzuu Amma.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Siha, Hussein Ramadhani, aliwapongeza walimu wa madrasa kwa maandalizi mazuri ya mashindano ya usomaji wa Qur’an Tukufu.

Katika mashindano hayo, washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu walipatiwa zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, huku washiriki wengine pia wakipewa zawadi za kifuta jasho kwa ushiriki wao.
Mwishooo…..

