Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso, amesema kuwa serikali kupitia Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha imeridhia kupandishwa hadhi kwa barabara ya Rhotia–Kambiva Simba–Selela Monduli.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, barabara hiyo sasa itaacha kuhudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kuanza kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mhe. Paresso ameyasema hayo leo Jumatatu, Machi 9, 2026, katika mkutano wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha.

Amesema uamuzi huo utasaidia barabara hiyo kupata matengenezo na huduma za kila mwaka, hatua itakayorahisisha mawasiliano pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu District.
“Kwa sasa ukipita kwenye barabara ile kuna changamoto kubwa ya kupitika, ikiwemo tope na maji barabarani hali
inayosababisha mawasiliano kukatika. Lakini kwa azimio hili ninaamini barabara hiyo itafanyiwa matengenezo na wananchi wataondokana na adha wanazokumbana nazo kwa sasa,” amesema Mhe. Paresso.
Mahitaji ya Barabara za Lami Karatu
Mbali na hilo, Mhe. Paresso pia amezungumzia umuhimu wa kuongezwa kwa barabara za kiwango cha lami katika Mji wa Karatu. Amesema mji huo una umuhimu mkubwa katika sekta ya utalii, hivyo miundombinu bora ya barabara ni muhimu ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha huduma kwa wakazi na wageni.

Mbunge huyo ameahidi kuendelea kusukuma ajenda hiyo ili kuhakikisha Mji wa Karatu unapata barabara nyingi zaidi za lami katika siku zijazo.
Ombi kwa Waziri Mkuu.
Katika ziara ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, iliyofanyika hivi karibuni mkoani Arusha, Mhe. Paresso alimwasilisha ombi la kupandishwa hadhi kwa barabara hiyo.
Akijibu ombi hilo, Waziri Mkuu aliagiza uongozi wa Mkoa kupitia kikao cha Bodi ya Barabara kujadili suala hilo na kutoa uamuzi, ambao sasa umezaa matunda kwa kuridhia kupandishwa hadhi kwa barabara hiyo.
Matokeo Yanayotarajiwa.
Kupandishwa hadhi kwa barabara ya Rhotia–Kambiva Simba–Selela Monduli kunatarajiwa kuboresha usafiri na usafirishaji, kurahisisha shughuli za kiuchumi, pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu na maeneo ya jirani
Mwisho …

