Na Geofrwy Stephen Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, amesisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano wa dhati kati ya viongozi na wananchi katika kuhakikisha utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo mkoani humo. Amewahimiza Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Meya wa Jiji, pamoja na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa kushirikiana kwa karibu katika kusimamia miradi muhimu ikiwemo ujenzi na matengenezo ya barabara za kiwango cha lami na changarawe.
Akizungumza Jumatatu, Machi 9, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 51 wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, Makalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, aliwashukuru viongozi na watendaji katika ngazi mbalimbali kwa ushirikiano wao tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.


Alisisitiza kuwa mshikamano huo ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa maono na dhamira ya maendeleo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Makalla alieleza kuwa uongozi wa mkoa utaendelea kuhakikisha miradi ya miundombinu, hususan barabara, inatekelezwa kwa ufanisi ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Alitoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara Tanzania, Tanzania National Roads Agency (TANROADS), kuongeza matumizi ya Mabaraza ya Madiwani kama jukwaa muhimu la kupokea na kujadili changamoto za barabara kutoka kwa madiwani wanaowakilisha kata mbalimbali.



Kwa mujibu wa Makalla, kupitia mabaraza hayo mahitaji halisi ya wananchi yanaweza kutambuliwa kwa urahisi, na hivyo kusaidia kupanga vipaumbele sahihi vya ujenzi na ukarabati wa barabara katika maeneo yao.
“Ni kupitia vikao kama hivi ndipo tunaweza kuazimia barabara zipi zipandishwe hadhi na zipi zijengwe kwa kiwango cha lami, kulingana na mahitaji ya wananchi na maelekezo ya serikali,” alisema Makalla.
Baadhi ya barabara zilizotajwa kupewa kipaumbele ni pamoja na barabara ya kuingia Hospitali ya Wilaya ya Arusha DC, Moshono–ByPass, Karatu–Eyasi, pamoja na Longido–Siha, hatua inayolenga kupunguza changamoto za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Katika mkutano huo, wajumbe pia walipokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti za taasisi zinazohusika na miundombinu ya barabara, ikiwemo TARURA, Tanzania National Roads Agency (TANROADS) na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026. Aidha,



walipitia mpango kazi wa mwaka 2025/2026 pamoja na kujadili bajeti ya matengenezo ya barabara na utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhusu ujenzi wa barabara mpya za lami na upandishaji hadhi wa baadhi ya barabara.
Hatua hizo zinaonekana kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara, ambayo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Mwishoo.

