Na Mwandishi .Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko, ameagiza Afisa Ardhi wa zamani wa wilaya hiyo ambaye kwa sasa anafanya kazi mkoani Singida atafutwe na kuletwa wilayani Hai kujibu tuhuma za kuondoka na fedha za mwananchi aliyetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Agizo hilo limetolewa leo Machi 6, 2026, wakati Mkuu huyo wa Wilaya alipoanza kushughulikia kero za wananchi zilizowasilishwa mbele ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba wakati wa ziara yake wilayani Hai.

Kero 27 za Wananchi Zaanza Kutafutiwa Ufumbuzi
Bomboko amesema jumla ya kero 27 za wananchi zilizowasilishwa wakati wa mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu zimeanza kufanyiwa kazi ili kupatiwa ufumbuzi.
Akizungumza mbele ya wananchi waliofika ofisini kwake kuwasilisha changamoto mbalimbali zikiwemo za migogoro ya ardhi na mirathi, Bomboko aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ya wilaya itahakikisha kero zote zinashughulikiwa.
“Ni kweli zile kero zilizowasilishwa alipokuja Waziri Mkuu zilipokelewa. Baadhi tayari tumeanza kuzifanyia kazi, na zingine tumeelekezwa kwenda kuzisikiliza moja kwa moja kwenye maeneo husika. Jumla yake zilikuwa kero 27,” amesema Bomboko.
Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi waliwasilisha kero zao kwa kuzungumza moja kwa moja wakati wa mkutano wa hadhara, huku wengine wakiziandika na kuziwasilisha kwa maandishi.


Utaratibu Mpya wa Kusikiliza Kero.
Mkuu huyo wa Wilaya pia amesema wameanzisha utaratibu mpya wa kusikiliza kero za wananchi kila Alhamisi, ambapo viongozi wa wilaya watakuwa wanazunguka katika tarafa mbalimbali kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.
Alisema utaratibu huo unalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuhakikisha kero zao zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Kisa cha Mwananchi Aliyetoa Ardhi Kujenga Shule.
Miongoni mwa kero zilizowasilishwa kwa Waziri Mkuu ni ya mwananchi Frank John, mkazi wa kata ya Bomang’ombe, ambaye anadai hakulipwa fedha baada ya kutoa eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Gezaulole mwaka 2012.
Frank amesema alitoa ardhi hiyo kwa hiari ili kusaidia watoto wa eneo hilo kupata elimu, baada ya kuahidiwa kulipwa fidia, lakini hadi sasa hajalipwa.
Amedai kuwa utaratibu huo ulisimamiwa na Afisa Ardhi wa kipindi hicho ambaye kwa sasa anafanya kazi katika halmashauri moja mkoani Singida.
DC Aagiza Afisa Huyo Aletwe Hai.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Bomboko aliagiza Afisa huyo atafutwe na kuletwa wilayani Hai ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Ni kweli aletwe hapa aje ajibu tuhuma zake. Atatafutwa kupitia Mkurugenzi wetu ambaye atawasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri aliyopo mkoani Singida,” amesema Bomboko.
Amesema Afisa huyo tayari aliwahi kupigiwa simu kuhusu suala hilo lakini alidai atafika kwa utaratibu rasmi ikiwa ni pamoja na kuandikiwa barua na kutumiwa nauli.
Bomboko amesema ofisi yake ipo tayari hata kumtumia nauli na fedha za matumizi ya njiani ili aweze kufika na kujibu tuhuma hizo.
Diwani Apongeza Hatua Hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bomang’ombe, Evord Njau, amepongeza hatua ya kuanza kushughulikia kero zilizowasilishwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu.
Amesema wananchi wa wilaya hiyo wameanza kuona matokeo ya ziara ya Waziri Mkuu.
“Ni kweli ziara ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba tumeanza kuona matunda yake ndani ya wilaya hii. Baadhi ya kero zilizokabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya zimeanza kushughulikiwa,” amesema Njau.
Mwishoo.

