Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) limemuingiza rasmi kazini Askofu Dk. Philemon Mollel, maarufu kwa jina la Monaban, kuwa Msaidizi wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Oscar Olutu, katika Parokia ya Ngulelo jijini Arusha.
Ibada ya kumuingiza kazini Askofu Mollel ilifanyika katika kanisa la Ngulelo, Arusha, na kuhudhuriwa na waumini mbalimbali, maaskofu, mbali mbali wakiwemo na wachungaji, viongozi wa serikali pamoja na wageni waalikwa kutoka mikoa zaidi ya 21 .
Askofu Mollel Aweka Nadhiri ya Utumishi
Katika ibada hiyo, Askofu Dk. Mollel aliweka nadhiri kwa kuahidi kutimiza majukumu yake kwa uaminifu na bila ubaguzi, huku akimuomba Mungu amsaidie katika nafasi hiyo mpya ya utumishi.
“Mimi Askofu Mollel naahidi kuweka nadhiri hii kwa Mungu na kuwatumikia waumini wa kanisa hili bila unabaguzi. Naomba Mungu anisaidie katika jukumu hili la kiutumishi,” alisema.
Baada ya nadhiri hiyo, maaskofu waliokuwepo walimbariki rasmi kwa ajili ya kuanza majukumu yake.
Askofu Mkuu Olutu Awasihi Waumini na Viongozi wa Dini
Kabla ya kumuingiza kazini, Askofu Mkuu wa KKAM, Oscar Olutu, aliwahimiza waumini kutosahau walipotoka na kusimama imara katika imani yao.
Katika mahubiri yake, alisisitiza viongozi wa dini kutokuwa waoga katika kuhubiri neno la Mungu na kutompa shetani nafasi ya kuleta uongo.
Alieleza kuwa Mungu ndiye anayejua imani ya kila mtu na kwamba mambo makubwa yanaweza kutokea kupitia imani ya kweli. Pia alimkumbusha Askofu Mollel kufanya kazi kwa ujasiri, akisema Mungu hafanyi kazi na watu waoga.
Historia na Ukuaji wa KKAM
Askofu Olutu alieleza kuwa kanisa hilo lilianzishwa mwaka 1999 likianza na parokia mbili — Himo na Uchira, zilizopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa sasa, KKAM lina zaidi ya parokia 136, waumini zaidi ya 801, wachungaji na mashemasi 160 pamoja na dayosisi nane.
Aidha, aliomba kanisa hilo lishirikishwe katika vikao vya kiserikali, kupatiwa kiwanja mkoani Dodoma, pamoja na kujengewa uzio katika eneo lao lililopo Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani Arusha.
Serikali Yatoa Ahadi ya Kushughulikia Maombi
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi, Ofisa Tarafa wa Moshono, Dominick Njunwa, alisema maombi yaliyotolewa yatawasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ili yafanyiwe kazi.
Alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.
Mwishooo…
