TAARIFA YA KUSIKITISHA:
Mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Abdilah Musa maarufu kama Banjo, amefariki dunia baada ya mwili wake kukutwa katika eneo la Bereko, wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Banjo, ambaye alikuwa mkazi wa Sanawari jijini Arusha, aliripotiwa kutoweka Februari 12 baada ya kwenda kufanya mazoezi ya viungo (gym) katika jengo la Ngorongoro, Arusha. Kwa mujibu wa taarifa za familia, watu wasiojulikana walifika eneo hilo na kuondoka naye, hali iliyozua taharuki na kuanza kwa juhudi za kumtafuta bila mafanikio.

Akizungumza kwa masikitiko, mtoto wa marehemu, Mussa Abdilah, amesema walipokea simu ikiwataarifu kuhusu kupatikana kwa mwili wa mwanaume pembezoni mwa barabara katika eneo la Bereko, Kondoa. Familia ilielekea eneo hilo na kuthibitisha kuwa mwili huo ulikuwa wa baba yao.
Mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umeharibika vibaya, hali inayoashiria uwezekano wa kufanyiwa ukatili kabla ya kifo chake.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo pamoja na kuwabaini waliohusika. Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu watuhumiwa au chanzo cha tukio hilo.
Kifo cha Banjo kimeacha simanzi kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na jamii ya wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha.
Tutaendelea kuwafahamisha wasomaji wetu kadri taarifa zaidi zitakavyopatikana kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama.


