JMAT SIHA YAFANYA KAMPENI YA UCHANGIAJI DAMU KUADHIMISHA MARIDHIANO DAY, YAKUSANYA CHUPA 75 ZA DAMU.

Geofrey Stephen
3 Min Read

katika kuadhimisha Maridhiano Day, Jumuhiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Siha mkoani Siha District imefanya kampeni ya uchangiaji damu kama sehemu ya juhudi za kuunga mkono Serikali katika kuokoa maisha na kuboresha afya ya jamii.

Kampeni hiyo ililenga kuongeza upatikanaji wa damu salama wilayani humo, ambapo jumla ya chupa 75 za damu zilikusanywa. Zoezi hilo lilifanyika katika maeneo mbalimbali, likihitimishwa Februari 13, 2026, katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali pamoja na wajumbe wa JMAT kutoka maeneo tofauti ya wilaya hiyo.

Habari Picha 7086
Habari Picha 7085

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Katibu wa JMAT Wilaya ya Siha, Hamisi Ramadhani, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuongeza upatikanaji wa damu salama ili kunusuru maisha ya wajawazito wanaohitaji damu wakati wa kujifungua, waathirika wa ajali pamoja na wagonjwa wengine wenye uhitaji.
“Katika maadhimisho haya, tuliona ni muhimu kuunga mkono juhudi za Serikali. Tunajivunia kuendesha zoezi hili la uchangiaji damu kwa lengo la kuokoa maisha,” amesema Hamisi.

Mbali na zoezi la uchangiaji damu, JMAT pia imeendesha shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kupanda miti katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Hospitali ya Wilaya ya Siha.
Aidha, JMAT imeendelea kutoa elimu ya kuzuia na kutatua migogoro katika jamii, baina ya watu, taasisi na makundi mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha amani katika wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma ya Damu Wilaya ya Siha, Jeremy Marck, alisema wilaya hiyo inahitaji kukusanya wastani wa chupa 46 za damu kila mwezi ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa, waathirika wa ajali, wajawazito na watoto wenye upungufu wa damu.

Nsubili Mwakapeje, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, aliipongeza JMAT kwa kuona umuhimu wa kuandaa kampeni hiyo, akisema ni mchango mkubwa katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya. Pia alitaja kutembelea wagonjwa, kuwafariji na kuwaombea kuwa ni kitendo cha huruma na mfano wa kuigwa.

Katika hafla hiyo, shukrani pia zilitolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuimarisha miundombinu ya afya, ikiwemo ujenzi wa majengo ya hospitali, kuongeza bajeti ya dawa na kuongeza idadi ya watumishi wa afya.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha, Jane Chalamila, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Christopher Timbuka, aliipongeza JMAT kwa mchango wake katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kuimarisha usalama na amani wilayani humo.

Habari Picha 7087

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JMAT, Jones Mola, alisema changamoto zilizobainishwa zitafanyiwa kazi, ikiwemo kuwajengea uwezo wajumbe kupitia mafunzo maalum na kuhakikisha wanapatiwa vitambulisho rasmi vya utendaji.

Habari Picha 7088
Habari Picha 7089

Maadhimisho ya Maridhiano Day yanatarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Mwanza Machi 4, 2026.

 

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment