Na Mwandi wa A24tv Siha
Katika kuadhimisha Maridhiano Day, Jumuhiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro imefanya kampeni ya uchangiaji damu kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuokoa maisha na kuboresha afya ya jamii.
Zoezi la ukusanyaji damu lilifanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, likihitimishwa Februari 13, 2026, katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Serikali pamoja na wajumbe wa JMAT kutoka maeneo tofauti ya wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa JMAT Wilaya ya Siha, Hamisi Ramadhani, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuongeza upatikanaji wa damu salama ili kunusuru maisha ya wajawazito wanaohitaji damu wakati wa kujifungua, waathirika wa ajali pamoja na wagonjwa wenye upungufu wa damu.
“Katika maadhimisho haya, tumeona ni muhimu kuunga mkono juhudi za Serikali. Tunajivunia kuendesha zoezi hili la uchangiaji damu kwa ajili ya kuokoa maisha,” alisema Hamisi.


Mbali na uchangiaji damu, JMAT pia ilitoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kupanda miti katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika viwanja vya hospitali hiyo. Aidha, jumuiya hiyo imeendelea kutoa elimu ya kuzuia migogoro katika jamii, taasisi na makundi mbalimbali kwa lengo la kudumisha amani ndani ya wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Mratibu wa Huduma ya Damu Wilaya ya Siha, Jeremy Marck, alisema wilaya inahitaji kukusanya angalau chupa 46 za damu kila mwezi ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa, wakiwemo waathirika wa ajali, wajawazito na watoto wenye changamoto ya upungufu wa damu.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, Nsubili Mwakapeje, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya, aliipongeza JMAT kwa kuandaa kampeni hiyo na kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya. Alisema pia matendo ya kutembelea wagonjwa, kuwafariji na kuwaombea ni ya kuigwa.
Viongozi wengine waliotoa pongezi ni pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha, Jane Chalamila, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Christopher Timbuka, ambaye alisema kazi inayofanywa na JMAT imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mshikamano na amani wilayani humo.
Mwenyekiti wa JMAT, Jones Mola, alisema jumuiya hiyo itaendelea kushughulikia changamoto zilizobainishwa, ikiwemo kuwajengea uwezo wajumbe wake kupitia semina maalum pamoja na kuwapatia vitambulisho rasmi ili kuboresha utendaji wao.


Kwa ujumla, maadhimisho ya Maridhiano Day yamekuwa chachu ya kuimarisha mshikamano wa jamii, kuboresha huduma za afya na kuendeleza juhudi za kulinda amani na utulivu katika Wilaya ya Siha.
Mwisho …….



