MAIPAC NA PRESS UNLIMITED WAIMARISHA UANDISHI WA AMANI NCHINI.

Geofrey Stephen
4 Min Read

Wanahabari Watakiwa Kuandika Habari za Amani na Kuzingatia Usalama Wao
Mwandishi Wetu

Taasisi ya Waandishi wa Habari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imetoa mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini kuhusu namna ya kuandika habari zinazochochea amani pamoja na kulinda usalama wao wanapotekeleza majukumu yao, hasa wakati wa migogoro.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha wanahabari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Mara, Manyara, Mbeya na Arusha, na yalidhaminiwa na shirika la kimataifa la Press Unlimited.

Msisitizo wa Uandishi wa Amani.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, aliwataka wanahabari kuandika habari zinazohamasisha amani na mshikamano wa jamii badala ya kuchochea migogoro.
Alisema kuwa habari za upande mmoja zisizozingatia maadili ya taaluma na maslahi mapana ya umma zimekuwa zikichangia kuibuka au kuongezeka kwa migogoro katika jamii.

Habari Picha 6928
Habari Picha 6929

“Ni muhimu kujiuliza habari ina madhara gani na ina faida gani kwa jamii. Tusiwe na upendeleo katika uandishi wetu na tuzingatie tahadhari za kiusalama, hususan tunapotumia vyombo vya kidijitali pamoja na kulinda usalama binafsi,” alisema Juma.
Aidha, aliwahimiza wanahabari kufanya uchambuzi wa kina kabla na baada ya kuchapisha habari ili kuhakikisha taarifa wanazotoa hazileti madhara kwa jamii wala kwao wenyewe.

Kuzingatia Sheria za Habari.

Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea John Sendodo alitoa mada kuhusu sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya habari nchini. Aliwataka wanahabari kuzifahamu na kuzizingatia sheria hizo hata pale wanapoona zina mapungufu.

Baadhi ya sheria alizozitaja ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, pamoja na Kanuni za Maudhui ya Mitandaoni.

Habari Picha 6930
Habari Picha 6931
“Kuna sheria kadhaa ambazo ni muhimu sana kwa wanahabari kuzijua. Tusome, tuelewe na tufanye kazi kwa kuzingatia misingi ya kisheria bila kuvunja sheria, huku tukitekeleza wajibu wetu kwa weledi,” alisisitiza Sendodo, ambaye pia anashirikiana na shirika la kimataifa la Protection Africa.

Maadili ya Uandishi na Ubora wa Habari.

Mmiliki wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Fanikiwa kilichopo Arusha, Joseph Mayagilla, alieleza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote wa utekelezaji wa majukumu ya uandishi.
Alisema kuwa kuongezeka kwa habari za upande mmoja na uandishi usiozingatia maadili kumeleta madhara katika jamii.
Mayagilla alipendekeza kurejeshwa kwa madawati maalum ndani ya vyombo vya habari, ikiwemo madawati ya habari za uchunguzi, amani na maendeleo, uchumi na mengineyo. Alieleza kuwa madawati hayo yakiongozwa na waandishi wabobezi yataongeza ubora na weledi wa habari.

Habari Picha 6932
Habari Picha 6933

Afya ya Akili kwa Wanahabari.

Mtaalamu wa saikolojia, Ester Cornelio, aliwataka wanahabari wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutafuta msaada wa kitaalamu badala ya kujifungia au kutumia njia zisizofaa kama vile unywaji wa pombe kupita kiasi au uvutaji wa sigara.
Alisema msongo wa mawazo (trauma) hauondolewi kwa matumizi ya vileo au sigara, bali kwa kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.

Cornelio alibainisha kuwa wanaume wamekuwa wahanga zaidi wa msongo wa mawazo kwa sababu mara nyingi hushindwa kueleza hisia zao, tofauti na wanawake ambao huwa wazi zaidi kuzungumza.

Habari Picha 6934
Habari Picha 6935

Wito wa Mafunzo Endelevu.

Wakichangia mada, wanahabari Tausi Mbowe, Meneja wa Dawati la Kidijitali Star TV, na Anthony Mayunga kutoka Serengeti Media, walisisitiza umuhimu wa kuimarisha maadili ya uandishi pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kuhusu sheria na afya ya akili kwa wanahabari.

Wanahabari wengine waliochangia ni Elizabeth Nyivambe (Mbeya), Muta Robert (Geita) na Zakaria Mtigandi (Manyara), ambao walieleza umuhimu wa kuendeleza mafunzo hususan katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na masuala ya usalama wa wanahabari.

Habari Picha 6936
Habari Picha 6937

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment