ARUSHA YAJIPANGA KIMATAIFA: RC MAKALLA ATANGAZA KAMATI 7 MAALUM ZA AFCON 2027

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, ametangaza rasmi kuundwa kwa kamati saba maalum zitakazosimamia maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, akieleza kuwa hatua hiyo ni kielelezo cha utayari wa mkoa huo kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya soka barani Afrika.

Akizungumza leo Jumanne, Februari 4, 2026, mbele ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala, Waganga Wakuu pamoja na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Makalla alisema maandalizi hayo yanapaswa kufanyika kwa weledi, mshikamano na uwajibikaji wa hali ya juu.

Habari Picha 6652
Habari Picha 6651

Alimuelekeza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa kuratibu uundwaji wa kamati hizo saba ambazo ni:

Kamati ya Usalama
Kamati ya Itifaki na Mapokezi
Kamati ya Habari, Mawasiliano na Hamasa
Kamati ya Afya
Kamati ya Malazi
Kamati ya Miundombinu
Kamati ya Utalii na Ukarimu.

Kwa mujibu wa RC Makalla, kamati hizo zitakuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha Arusha inajiandaa kikamilifu kupokea wageni, timu, viongozi pamoja na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na nje ya bara hilo.

Fursa za Kiuchumi Zang’aa
Katika hotuba yake, Mhe. Makalla aliwahimiza wananchi wa Arusha, wamiliki wa hoteli, makampuni ya utalii pamoja na watoa huduma za usafirishaji kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi zitakazoambatana na ujio wa AFCON 2027.

Alisisitiza kuwa michuano hiyo si tukio la michezo pekee, bali pia ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa ndani kupitia ukuaji wa utalii, biashara na ajira.

Aidha, aliliagiza Jiji la Arusha kuongeza jitihada za kuimarisha usafi wa mazingira, kuboresha miundombinu ya jiji na kupendezesha mandhari ili liendane na hadhi ya tukio la kimataifa.

Shukrani kwa Rais Samia.

Habari Picha 6654
Habari Picha 6653

RC Makalla alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuichagua Arusha kuwa miongoni mwa maeneo yatakayohusika na AFCON 2027.

Pia alitambua juhudi za Serikali katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa daraja la Category 4 wenye viwango vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Habari Picha 6655

Aliahidi kuwa uongozi wa mkoa utashirikiana kwa karibu na wataalamu wa ngazi zote kusimamia maandalizi hayo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha taifa linapata sifa kimataifa, huku wananchi wakinufaika moja kwa moja kiuchumi.

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment