Siha, Kilimanjaro
Serikali ya Wilaya ya Siha imeunda timu maalum kushughulikia kero za wafugaji zinazohusiana na upatikanaji wa maeneo ya malisho katika eneo la Ranchi ya Taifa (NARCO) – West Kilimanjaro.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha, Jane Chalamila, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, alipokutana na wafugaji waliokusanyika katika eneo la ranchi hiyo wakitaka maombi yao ya kuongezewa maeneo ya malisho kusikilizwa.

Akizungumza na wafugaji hao Januari 30, 2023, mara baada ya kusikiliza kero zao, Chalamila aliwataka kuchagua wawakilishi wanaowaamini (Maolegwani) watakaounda timu itakayoshirikiana na Serikali ya Wilaya kufuatilia na kutatua changamoto hizo.
“Sisi kama Serikali ya Wilaya, pamoja na wawakilishi mtakaowachagua, tunachukua kero zote mlizozitoa na kuzipeleka kwa mwekezaji ambaye ni NARCO, hadi makao makuu Dodoma, ili tupate majibu rasmi na kuwaletea nyinyi,” alisema Chalamila.
Kero Kuu: Kuongezewa Maeneo ya Malisho
Moja ya kero kubwa iliyowasilishwa ni ombi la wafugaji la kuongezewa eneo la malisho, ambalo wanasema waliwasilisha NARCO makao makuu tangu mwaka 2023 lakini halijapatiwa majibu hadi sasa.
Pia, walieleza malalamiko kuhusu uwepo wa mwekezaji mmoja kutoka Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha, ambaye wanadai amepewa eneo hilo huku wakihisi kuwa kuna maeneo ya kutosha ya malisho Longido, hivyo uwepo wake Siha unawanyima nafasi wafugaji wa eneo hilo.
Chalamila aliwahakikishia wafugaji kuwa Serikali imesikia hoja zao na kuwaomba wawe na subira wakati mchakato wa kushughulikia suala hilo ukiendelea.

Wafugaji Walalamikia Faini Kubwa
Mmoja wa wafugaji, Yeyeni Mollel, alisema kwa muda mrefu kulikuwa na uhusiano mzuri kati ya wafugaji na NARCO bila migogoro mikubwa.
Hata hivyo, alidai mwekezaji huyo mpya amekuwa akiwatoza faini kubwa wanapokamatwa mifugo yao, ambapo ng’ombe mmoja hutozwa shilingi 50,000.
“Hii ni kama unyanyasaji. Tunaomba Serikali itusaidie. Tuko tayari hata kulipia eneo ili mifugo yetu ipate malisho, kwa sababu sasa inakufa kwa njaa,” alisema Mollel.

Vijiji Vingi Vinategemea NARCO
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Siha, Mathayo Lengere, alisema eneo la NARCO West Kilimanjaro limezungukwa na zaidi ya vijiji kumi vya wafugaji ambavyo havina maeneo ya kutosha ya malisho.
Alivitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni Magadini, Ndinyika, Mawasiliano na Lekrumuni, ambavyo vina chini ya ekari 1,000 huku idadi ya mifugo ikiwa kubwa kuliko uwezo wa ardhi.
Lengere alisema aliwahi kuandika barua za maombi ya kuongezewa maeneo ya malisho kwenda Bodi ya NARCO West Kilimanjaro na pia makao makuu Dodoma, lakini hadi sasa hawajapata majibu

Kwa mujibu wake, zaidi ya wafugaji 15,000 wanategemea suluhisho la suala hilo na wako tayari kulipia maeneo ya malisho iwapo watapewa fursa.
NARCO Watoa Majibu
Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, Meneja wa NARCO West Kilimanjaro, Lwimiko Mwansonga, alisema majibu ya mwisho kuhusu suala hilo yanatolewa na makao makuu ya NARCO Dodoma .
Mwisho …



