Arusha, Januari 24, 2026 — Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Mhe. Maxmillian Matle Iranqhe, amezindua rasmi awamu ya tatu ya kampeni ya usafi wa mazingira ijulikanayo kama “Ng’arisha Jiji”, katika Kata ya Daraja II. Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha usafi wa mazingira.


katika maeneo yote ya Jiji la Arusha.
Uzinduzi huo uliambatana na zoezi la vitendo la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo la Kituo cha Afya Daraja II, ambapo wananchi, viongozi wa kata pamoja na wadau mbalimbali walishiriki kikamilifu.
Akihutubia wananchi waliojitokeza kushiriki,
Meya Maxmillian alisisitiza umuhimu wa kufanya usafi wa mazingira kuwa utamaduni wa kila siku, badala ya kusubiri siku maalum pekee kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya maeneo.


“Usafi wa mazingira usiwe wa Jumamosi pekee.
Unapaswa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku — nyumbani, maeneo ya biashara na katika taasisi zetu,” alisisitiza Meya huyo.
Aidha, aliwaelekeza Watendaji wa Kata kuhakikisha wanawasimamia Maafisa Afya katika kusimamia kikamilifu zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo yao mara kwa mara.
Pia alihimiza utoaji wa elimu kwa wananchi.
kuhusu utunzaji wa mazingira, hususan kufanya usafi wa maeneo yao ya biashara na makazi:
Kabla ya kufungua biashara asubuhi.
Jioni baada ya kumaliza shughuli za biashara
Kampeni ya “Ng’arisha Jiji” imekuwa sehemu ya mkakati wa Jiji la Arusha wa kuboresha afya ya jamii, kuzuia magonjwa yatokanayo na uchafu, pamoja na kulifanya jiji kuwa safi na lenye mandhari ya kuvutia.


Wananchi wametakiwa kuendelea kushirikiana na viongozi wao ili kuhakikisha lengo la kuwa na Arusha safi, salama na lenye hadhi ya jiji la kisasa linafikiwa.
Mwisho .



