TADB Yatoa Elimu ya Kifedha kwa Wananchi na Wanafunzi Tanga

a24tv
2 Min Read

Na Lucy Ngowi

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi na wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga jamii yenye uelewa mzuri wa masuala ya fedha na maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho hayo yanayoendelea mkoani Tanga, katika viwanja vya Usagara, Ofisa Maendeleo wa Biashara wa TADB Kanda ya Kaskazini, Irene Kasegezya, alisema benki hiyo imekuwa ikitoa elimu ya kifedha kwa makundi mbalimbali tangu kuanza kwa maonyesho hayo Januari 19, 2026.

Kasegezya alisema hadi sasa TADB imewahudumia wananchi wengi, wakiwemo wanafunzi zaidi ya 200, waliopatiwa elimu ya kifedha itakayowasaidia kujenga msingi imara wa usimamizi wa fedha kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Alisema elimu hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi nidhamu ya kifedha mapema na kuwaandaa kuwa na desturi chanya za kifedha.

Aliongeza kuwa wananchi waliotembelea banda la TADB wamepata fursa ya kushiriki mafunzo kuhusu upangaji wa matumizi, utunzaji wa kumbukumbu za fedha pamoja na maandalizi ya kupata mikopo.

Aidha, alibainisha kuwa elimu ya kifedha ni muhimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kwani huwasaidia kupanga shughuli zao kiuchumi na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa yanafanyika mkoani Tanga chini ya kaulimbiu isemayo ‘Elimu ya Kifedha ni Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.’.

Kasegezya aliwahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda la TADB ili kupata elimu, ushauri wa kitaalamu na taarifa kuhusu huduma za benki hiyo.

Share This Article
Leave a Comment